Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita kuwa kushirikiana na Taasisi
ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMIVITA) na Benki Kuu ya Tanzania imeendesha
mafunzo ya utambuzi wa noti kwa Watu wenye Ulemavu hususani Viziwi.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati Dkt Doto Biteko, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis leo Mei 10, 2024 Wilayani
Bukombe mkoani Geita, amesema Serikali imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya
watu wenye Ulemavu katika masuala ya elimu, uwezeshaji kiuchumi, afya, ajira,
nyenzo za kujimudu pamoja na mafunzo ya ufundi stadi kwa lengo la kuwawezesha
na kuwaunganisha na fursa zilizopo katika jamii.
Ameongeza Serikali inatambua kuwa watu wenye Ulemavu wakiwemo
Viziwi bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazosababisha wengi wao
kutofikia malengo yao. Kutokana na hali hiyo, Serikali inaendelea kuchukua
hatua mbalimbali sambamba na kutekeleza matakwa ya Sheria ya watu wenye Ulemavu
Namba 9 ya mwaka 2010 na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu
kupitia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020 - 2025.
"Nitumie fursa hii kuwashukuru wadau wa maendeleo
mlioshiriki kuandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo Watu wenye Ulemavu na ni dhahiri
mmekuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinazolenga kumuwezesha kila mwananchi
na hali yake kupata huduma stahiki na kwa wakati," amesisitiza Naibu
Waziri Mwanaidi.
Aidha amelitaka kundi hilo kuchangamkia fursa za fedha
zinazotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum inayotoa mikopo yenye masharti nafuu kupitia benki ya NMB kwa
wafanyabiashara wadogo ambapo Mheshimiwa Rais ametoa bilioni 18.5 kwa ajili ya
kuwakopesha wafanyabiashara wadogo.
"Fikeni
Halmashauri, hususani Ofisi za Maendeleo ya Jamii ili waweze kuwapa utaratibu
wa kupata mikopo hiyo.Pia, ninawasihi mjisajili na kupata vitambulisho vya
wajasiriamali wadogo (Maarufu MACHINGA) mara vitakapoanza kutolewa ili muweze
kukopesheka katika taasisi za fedha na Mamlaka za Serikali za Mitaa hususani
katika mikopo ya 10% (4-4-2) ambayo Mheshimiwa Rais ameelekeza ianze kutolewa
kuanzia mwaka wa fedha 2024/25 kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu,"
amesema Naibu Waziri Mwanaidi.
Kwa upande wake Katibu wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi
Tanzania (TAMIVITA) Wilaya ya Bukombe
Kevin Nyema ameishukuru Serikali kwa kuwezesha mafunzo hayo muhimu
yatakayowasaidia kutambua noti wakati wa shughuli zao mbalimbali za kiuchumi na
kuwapa fursa zaidi ya kushiriki pia katika shughuli hizo kikamilifu.
"Asante sana Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa
kuendelea kutujali sisi watu wenye ulemavu, wadau mbalimbali wakiwemo Benki Kuu
ya Tanzania kwa kuwezesha mafunzo haya," alisisitiza Nyema.
Mafunzo ya utambuzi wa noti kwa watu wenye ulemavu husani viziwi yanaratibiwa na Benki Kuu ya Tanzania kwa kuzingatia miongoni na kanuni mbalimbali za fedha nchini kwa lengo la kuwapa uwezo kundi hilo kukabiliana na changamoto za kifedha ikiwemo utapeli unaohusisha utoaji na upokeaji wa pesa zisizo halali.
0 Maoni