Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema Serikali itaendelea
kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma za saratani na vifaa tiba ili kutanua wigo wa huduma za Saratani nchini
na hivyo kuwezesha upatikanaji wa huduma
hizo kwa urahisi.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 2 Mei, 2024 wakati
akimwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika uzinduzi wa Kituo cha Matibabu ya Saratani cha Aga Khan,
Jijini Dar es Salaam.
“Serikali yetu imejipanga
kuboresha huduma za afya na kupambana na
magonjwa yasiyoambukiza na mfano wa juhudi hizi ni Serikali kutenga eneo
kilipojengwa kituo hiki ambacho kimepanga kuhudumia wagonjwa 100 kwa siku kwa matibabu ya mionzi,
wagonjwa 25 kwa siku kwa tiba za kemikali
na wagonjwa 25 kwa siku kwa uchunguzi wa saratani na huduma za chanjo.” Amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko ametoa rai kwa uongozi wa Hospitali hiyo
kuhakikisha wananchi wote bila kujali dini, kipato na itikadi zao wanapata
huduma hizo muhimu za afya.
Aidha, ameupongeza Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN)
kupitia Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan Tanzania kwa ushirikiano na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI)
pamoja na Kituo cha Tiba Bugando (BMC) kwa kubuni mradi shirikishi kati ya
sekta ya umma na sekta binafsi uitwao Mradi Mtambuka wa Saratani Tanzania
(TCCP) ambao unaunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na Saratani.
Ameeleza kuwa, mradi huo wenye thamani ya jumla ya Euro
milioni 13.3 (shilingi 35 bilioni) umekuwa na mafanikio mbalimbali ndani ya
miaka minne ya utekelezaji wake ikiwemo kutoa mafunzo kwa wahudumu 464 na
watumishi 400 ngazi ya jamii kuhusu huduma za Saratani.
Kupitia mradi huo wanajamii zaidi ya milioni 4.5 wamepewa
elimu kuhusu saratani, watu takriban 700,000 wamepimwa saratani na zaidi ya
wagonjwa wapya 39,093 kugunduliwa kuwa na saratani kupitia vipimo stahiki na
hivyo kuwawezesha kuanza kupata tiba stahiki.
Pamoja na pongezi hizo, Dkt. Biteko ametoa wito kwa Taasisi
mbalimbali za afya nchini kuhakikisha zinajikita pia kwenye kuzuia ugonjwa wa
saratani kwa njia mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya afya na lishe kwani wataalam
wanaamini kuwa magonjwa hayo yanaweza
kuepukika na hivyo kuepusha gharama kubwa zinazotumika kwenye matibabu.
Pia ametoa agizo kwa kituo hicho cha Aga Khan kushirikiana
na vituo vingine vya matibabu ya Saratani
nchini hususan Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ili kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji
madhubuti wa huduma za tiba za mionzi na hivyo kupunguza msongamano wa wagonjwa
Ocean Road.
Dkt. Biteko ameuhakikisha uongozi wa Hospitali ya Aga Khan
kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango wao katika utoaji wa huduma za
afya hasa kwenye magojwa yasiyoambukiza na kwamba ipo tayari kutoa ushirikiano
kwao muda wote.
Awali, Waziri wa
Afya, Mhe. Ummy Mwalimu alisema kuwa changamoto ya saratani nchini ni kubwa
ambapo kila mwaka kuna wagojwa wapya 40,000 huku vifo 27,000 na kwamba saratani
inayoongoza ni ya mlango wa kizazi kwa asilimia 23.5.
Amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya mapambano dhidi
ya saratani ikiwemo kuboresha miundombinu, kununua vifaa tiba vya kisasa na
kusomesha wataalam wa matibabu ya saratani ambapo mwaka huu ametoa shilingi Bilioni
10 kwa ajili ya kusomesha madaktari bingwa na madaktari wabobezi kwenye masuala
ya Saratani.
Amesema uboreshaji wa huduma za afya nchini unaendelea ili
kutimiza dhima ya Rais, Dkt. Samia ya kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha
utoaji wa huduma za kisasa za afya kwa wananchi ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Taasisi ya Huduma za Afya Aga Khan, Mwana Mfalme Bi. Zahra Aga Khan amesema kujengwa kwa kituo hicho ni ushahidi wa namna Tanzania inavyopiga hatua kwenye Sekta ya Afya kwa kutumia pia teknolojia ya hali ya juu ya kisasa kwenye matibabu.
0 Maoni