UWEPO WA KIMBUNGA "HIDAYA" KATIKA BAHARI YA HINDI
MASHARIKI MWA PWANI YA MTWARA
Dar es Salaam, 02 Mei 2024:
Kufuatia taarifa iliyotolewa jana tarehe 01 Mei, 2024 na
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa
katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya Mtwara, mgandamizo huo mdogo wa
hewa umeendelea kuimarika na kuwa kimbunga "HIDAYA" chenye nguvu ya
kati, kikiwa umbali wa takriban Kilomita 506 mashariki mwa pwani ya Mtwara.
Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini inaonesha
uwezekano mkubwa wa Kimbunga "HIDAYA", kusogea karibu kabisa na pwani
ya Tanzania kuanzia usiku wa leo tarehe 02 Mei 2024 na kuendelea kuwepo hadi
tarehe 06 mwezi Mei 2024. Hata hivyo, kimbunga hicho kinatarajiwa kupungua
nguvu baada ya tarehe 6 Mei 2024.
Uwepo wa kimbunga "HIDAYA" karibu na pwani ya nchi
yetu unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa chini ikiwa
ni pamoja na kusababisha vipindi vya mua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya
maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es
Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya jirani hususan
tarehe 3 Mei 2024 kwa maeneo ya pwani ya kusini (Lindi na Mtwara) na kusambaa
katika maeneo mengine ya ukanda wa pwani kuelekea tarehe 4 hadi 6 Mei 2024.
USHAURI: Wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha
na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa na pia
kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka TMA,
na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na
athari zinazoweza kujitokeza. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea
kufuatilia mwenendo wa kimbunga "HIDAYA" na athari zake kwa mifumo ya
hali ya hewa hapa chini na itaendelea kutoa taarifa mara kwa mara kila
inapobidi.
Imetolewa na: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
Mawasiliano yote yaelekezwe kwa:
Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Chuo
Kikuu cha Dodoma, Jengo la Utawala, Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu
Angavu, 1Mtaa wa CIVE, S.L.P 27, 41218 Dodoma; Simu: + 255 26 2962610: Nukushi:
+ 255 26 2962610 Barua pepe; met@meteo.go.tz; Tovuti: www.meteo.go.tz
(ISO 9001:2015 Certified in Aviation Services)
105A
0 Maoni