WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa yote
nchini waanze kufanya tathmini na kubainisha maeneo ambayo yatatumika kufanya
mazoezi kila Jumamosi.
“Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa waanze kufanya tathmini ya
maeneo waliyonayo na kutenga maeneo ya kufanyia mazoezi. Siyo lazima wafunge
barabara kama ilivyo kwa Dar e Salaam, wanaweza kuchagua uwanja mmoja walionao
ili kutekeleza agizo hilo.”
Ametoa wito huo Bungeni leo (Alhamisi, Mei 2, 2024) wakati
akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Kunti Majala kwenye kipindi cha maswali
ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambaye alitaka kujua Serikali ina mkakati gani
wa kuhakikisha mikoa yote inatekeleza agizo la kufanya mazoezi kila Jumamosi
ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.
“Ni kweli wiki iliyopita wakati wa mbio za kuchangisha fedha
kwa ajili ya watoto wenye usonji, Waziri wa Afya alisema Watanzania wengi wana
magonjwa mengi yasiyoambukiza ambayo yanatokana na mfumo wa maisha (lifestyle)
tulionao.”
“Dar es Salaam inaongoza kwa kuwa na vikundi vingi vya
jogging katika wilaya zake za Ilala, Kinondoni, Temeke, Ubungo na Kigamboni.
Tumeona ni muhimu tupange siku moja ili tuanze kufanya mazoezi. Niliagiza kila
Jumamosi, barabara ya kuanzia Coco Beach, kuja daraja la Tanzanite hadi ufukwe
wa Aga Khan ifungwe kuanzia saa 12 hadi saa 3 asubuhi ili kila mtu anayetaka
kufanya zoezi atumie fursa hiyo.”
Amesema kuna barabara nyingi za kufika katikati ya mji
ambazo zinaweza kutumika wakati barabara hizo zitakuwa zimefungwa ili kupisha
watu wanaofanya mazoezi hasa ikizingatiwa kuwa muda huo hakuna msongamano
mkubwa wa magari. “Maeneo ya uwanja wa Farasi, viwanja vya Gymkhana na Coco
Beach yatumike kuegesha magari kwa wale wanaotoka maeneo ya mbali kuja kufanya
mazoezi,” amesema.
Amewataka maaskari wa usalama barabarani wasimamie zoezi hilo na endapo italazimu, waruhusu magari ya kubeba wagonjwa, zimamoto, TANESCO na baiskeli za mazoezi kuwa ndiyo vyombo vitakavyotumia njia hiyo wakati imefungwa.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeweka
mpangokazi wa kutumia maji ya mvua kuwa vyanzo vya maji na kuyaelekeza kwa
wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.
“Serikali kupitia Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Maji
tayari zimeweka mpango kazi wa kutumia mabonde tuliyonayo na maji
yanayotiririka kwenye mabonde hayo na mifereji iliyosababishwa na mvua, kama
fursa kwa wananchi.”
Amesema kuwa Wizara ya Kilimo ipo katika mpango wa ujenzi wa
miradi mbalimbali ya umwagiliaji ambayo itahusisha uchimbaji wa mabwawa kwa
ajili ya kutumia maji ya mvua na kuyapeleka katika mifumo ya umwagiliaji.
“Wizara ya Mifugo pia itatumia fursa hiyo kutengeneza
mazingira mazuri kwa ajili ya wafugaji wetu kwa kujenga mabwawa ya kunyweshea
mifugo, pia Wizara ya Maji itajenga mabwawa ambayo yatakusanya maji ya
kuyapeleka katika maeneo yaliyo karibu.”
Amesema kuwa kwa mkoa wa Dodoma tayari Serikali imeshatenga
fedha na kutangaza zabuni ya kuziba maji katika eneo la Farkwa ili kuyatumia
maji hayo kwa ajili ya maeneo ya Dodoma mjini na Bahi. “Tunafanya hivyo kwenye
Mabonde ya Rufiji, Kilombero na Ruvuma.”
Alikuwa akijibu swali la Fatma Toufiq (Viti Maalum) ambaye alitaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kubadilisha maji ya mvua ili yatumike kama vyanzo vya maji.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni