Waziri wa Ardhi, Nyumba ya Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry
Silaa ametaja vipaumbele vitano vya wizara hiyo kuwahudumia Watanzania sekta ya
ardhi nchini kwa mwaka 2024/2025 na kuliomba Bunge lijadili na kuidhinisha Bajeti
ya Shilingi 171,372,508,000 ili kutekeleza majukumu ya wizara hiyo.
Akiwasilisha Bungeni Hotuba ya makadirio ya mapato na
matumizi ya wizara hiyo Mei 24, 2024 jijini Dodoma, Waziri Silaa amevitaja
vipaumbele hivyo kuwa ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa
ardhi mijini na vijijini, kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi na
kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa huduma na
upatikanaji wa taarifa za ardhi.
Vipaumble vingine ni kuhakikisha uwepo wa nyumba bora,
ukuaji wa sekta ya milki na maendeleo ya makazi kwa ajili ya maendeleo ya
kiuchumi na kijamii na kuimarisha mipaka ya kimataifa.
“Nawahimiza wananchi kote nchini kuendelea kutumia Ofisi za
Ardhi za Mikoa kupata huduma za umilikishaji wa ardhi na kuhakikisha
wanamilikishwa maeneo yao kwa mujibu wa sheria,” amesema Waziri Silaa.
Miongoni mwa majukumu ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi ambayo yatafanikisha vipaumbele vya wizara hiyo ni kuandaa
mipango ya matumizi ya ardhi, kusimamia upangaji wa miji na vijiji, kupima
ardhi na kutayarisha ramani, kutoa hati za kumiliki ardhi na hatimiliki za
kimila, kusajili hati za umiliki ardhi na nyaraka za kisheria pamoja na
kuthamini mali.
Majukumu mengine ni kuhamasisha na kuwezesha wananchi kuwa
na nyumba bora, kutatua migogoro ya ardhi na nyumba, kusimamia upatikanaji na
utunzaji wa kumbukumbu za ardhi, kusimamia ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali
yatokanayo na huduma za sekta ya ardhi, kusimamia Shirika la Nyumba la Taifa,
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Wakala wa Taifa wa Utafiti wa
Nyumba na Vifaa vya Ujenzi na Wakala wa Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni,
kusimamia uendeshaji wa Vyuo vya Ardhi vya Tabora na Morogoro na, kusimamia
maslahi na utendaji kazi wa watumishi wa sekta ya ardhi.
Aidha, Waziri Silaa amewapongeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini kwa ushirikiano wao wa karibu kwa Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa na wataalam.
Na. Eleuteri Mangi (WANMM) Dodoma
0 Maoni