WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa nchini
waakisi utashi wa kisiasa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia na
kutekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai.
“’Utashi wa kisiasa wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika kuboresha mfumo wa utoaji wa Haki Jinai lazima udhihirike kwenu
ninyi viongozi mlio karibu na wananchi. Hata hivyo, utashi huo hauwezi
kudhihirika kwenu iwapo hamtakuwa na nia ya dhati ya kubadilika na kisha
kuongoza mabadiliko kwenye maeneo mnayomwakilisha Mheshimiwa Rais wetu na
hususan katika kuhudumia wananchi,” amesema.
Ametoa wito huo leo (Jumatatu, Mei 6, 2024) wakati akifungua
warsha ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ya kuwajengea uelewa
kuhusu maboresho kwenye mfumo wa Haki Jinai na utoaji wa haki nchini kwenye
ukumbi wa mikutano wa Tume Huru ya Uchaguzi, uliopo Njedengwa, nje kidogo ya
Jiji la Dodoma.
Amesema sambamba na suala la utashi, ni lazima viongozi na
watendaji wa Serikali wawe na uelewa wa kutosha ili waweze kuyasimamia na
kuyatekeleza mapendekezo hayo.
Amesema malalamiko ya wananchi katika masuala kadhaa ndiyo
yaliyoweka msukumo kwa Mheshimiwa Rais kuunda Tume ya Haki Jinai na kuyakubali
mapendekezo yaliyotolewa na Tume hiyo na hatimaye kuigeuza kuwa Kamati ya
kuandaa mikakati utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.
“Hivyo basi, kwa kuwa ninyi ni wawakilishi wa Mheshimiwa
Rais katika maeneo yenu ya utawala, ni wajibu wenu kuhakikisha kuwa azma ya
Mheshimiwa Rais inatimia kwa kusimamia na kutekeleza mapendekezo yote
yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai,” amesisitiza.
Akitaja masuala yaliyolalamikiwa na wananchi, Waziri Mkuu
amesema utungaji wa baadhi ya sheria ndogo katika mamlaka zao ambazo aghalabu
hukinzana na sheria mama. “Mfano ni tozo zinazoanzishwa na halmashauri kama
vile ushuru wa mabango, kodi za maegesho na usimamizi wa matumizi ya maeneo ya
barabara zinasababisha mkanganyiko kwa wananchi kwa kuwajibishwa na chombo
zaidi ya kimoja,” amesema.
Masuala mengine ni migogoro ya ardhi, matumizi mabaya ya
madaraka ya ukamataji na desturi kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuambatana na
Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama katika ziara mbalimbali hata zile
zisizohitaji uwepo wa vyombo hivyo, hali ambayo imekuwa ikisababisha hofu kwa
wananchi na kuwafanya washindwe kufikisha mawazo na kero zao kwa viongozi hao.
Amewataka viongozi wote walioshiriki warsha hiyo wazingatie
maelezo yatakayotolewa ili kila mmoja akawe chachu ya mabadiliko ya kifikra,
kimtizamo na kiutendaji katika eneo lake. “Wakuu wa Mikoa na viongozi wote
mlioshiriki katika warsha hii, endeleeni kushirikiana na taasisi za Haki Jinai
katika utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ya kuboresha mfumo na
utendaji wa taasisi hizi.”
Amewataka wazingatie uwepo wa majengo na miundombinu muhimu kwa ajili ya taasisi za Haki Jinai katika maeneo mapya ya utawala (Wilaya) yaliyoanzishwa. “Kuna maeneo mengi mapya ya utawala bado huduma za Haki Jinai kama vile vituo vya Polisi na magereza hazijafika na wananchi wanapata taabu sana kuzifikia huduma hizo katika Wilaya mama ikiwemo kutembea au kusafiri kwa muda mrefu,” amesisitiza.
Mapema, Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo
Dugange alisema kuwa ofisi hiyo itasimamia utekelezaji wa maagizo na maelekezo
yatakayotolewa katika warsha hiyo ili dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kuona wananchi wanapata haki zao inafikiwa.
“Naomba nitumie nafasi hii kukuhakikishia kuwa yote ambayo
tutajifunza katika warsha hii na maelekezo yote ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu
utatupa tutahakikisha tunakwenda kuyatekeleza katika mikoa na halmashauri zetu
ili dhamira ya mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai yaweze kufikiwa.”
Naye, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed
Othman Chande alisema Kamati yao iliundwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Septemba 2023 ili kufanyia kazi ripoti ya Tume iliyokuwa na mapendekezo 333 ya
maboresho ya utendaji kazi wa taasisi za haki jinai katika maeneo mbalimbali.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa matukio ya uhalifu nchini
yanazidi kuongeza mwaka hadi mwaka na kwamba juhudi kubwa zinaelekezwa
kupambana na uhalifu badala ya kubaini na kuuzuia.
“Moja ya majukumu tuliyopewa kwenye kamati hii ni kuandaa
Mkakati wa Kitaifa wa Kubaini na Kuzuia Uhalifu unaotarajiwa kuwa nyenzo ya
utekelezaji wa taasisi na mamlaka zote zinazohusika ili kukabiliana na janga la
uhalifu nchini,” alisema na kuongeza kuwa viongozi na watendaji wote watakuwa
na jukumu la kusimamia utekelezaji wa mkakati huo utakaporidhiwa na Serikali
ili malengo yake yaweze kutimia.
Mada zinazowasilishwa kwenye warsha hiyo ni: Kujenga Uelewa wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai; Mfumo wa usimamizi, Kujenga Uelewa wa namna ya kutekeleza Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai; Mfumo wa usimamizi ufuatiliaji na uwajibikaji wa Viongozi na Watendaji na kuzingatia weledi, maadili na rushwa katika kuhakikisha upatikanaji wa haki.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni