WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka mamlaka zinazohusika
na usimamizi wa sekta ya habari ziendelee kusimamia vyombo vya habari
vizingatie maadili na kujiepusha na uchapishaji wa taarifa na picha
zinazochochea uvunjaji wa maadili, mila na desturi za Kitanzania.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na
wadau wa habari za mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ili kuhakikisha
kuwa sekta hiyo inaendelea kukua na kuchangia kuleta maendeleo kwa Taifa.
“Kupitia vyombo vya habari, hasa vya mitandao ya kijamii,
tumeweza kuwahabarisha wananchi kuhusu shughuli na mipango ya Serikali, na
kuhamasisha ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli na mipango
hiyo.”
Waziri Mkuu ametoa
kauli hiyo leo (Jumanne, Mei 21, 2024) katika Kongamano la Jumuiya ya
Wanahabari wa Mitandaoni ya Kijamii (JUMIKITA) kuhusu mafanikio ya miaka mitatu
ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye Ukumbi wa Chuo Kikuu cha
Dar Es Salaam.
Ameongeza kuwa
Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha Sheria na Miongozo
inayosimamia sekta ya habari ili kuweka mazingira wezeshi kwa wanahabari
kufanya kazi zao kwa uhuru na kwa kuzingatia maadili, tamaduni na haki za watu
wengine.
“...Katika kipindi hiki cha miaka mitatu toka Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani amewezesha kukua kwa sekta ya
habari na hasa ongezeko la watumiaji na
wasomaji wa habari kupitia mitandao ya simu.”
Aidha, Waziri Mkuu
amesema Serikali imeandaa Mkakati wa Mawasiliano wa Taifa ili kuhakikisha wadau
katika ngazi zote wanapata taarifa za kutosha na wanashiriki kikamilifu katika
maendeleo ya nchi na kuimarisha mawasiliano ya Serikali.
Awali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, Nape Nnauye ameilekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iandae
utaratibu wa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa waandishi wa habari za mitandaoni
ili kuwajengea uwezo wa kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili na utamaduni wa
Kitanzania.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JUMIKITA, Shaban Matwebe ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyosimamia ukuaji endelevu wa sekta ya habari nchini ikiwemo kuimarisha uhuru wa vyombo hivyo.
0 Maoni