Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry
Silaa amesema zoezi la urasimishaji linaloendelea maeneo mbalimbali nchini
litaboreshwa ili kuleta ufanisi.
Mhe. Silaa amesema hayo jana wakati wa semina kwa Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii kuhusu Utekelezaji Mradi
Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini (LTIP) hadi kufikia Mei 15, 2024
iliyofanyika kwenye ukumbi wa Samwel Sitta Bungeni jijini Dodoma.
Amesema, maboresho hayo ya zoezi la urasimishaji yatawafanya
wananchi kuelewa kuwa, kuishi eneo rasmi kama vile lile la mita za mraba 750
kuna faida zaidi ukilinganisha na kuishi eneo lenye ukubwa wa mita za mraba
1000 lisilo rasmi.
“Wananchi waelewe kuishi eneo rasmi lenye square mita 750
kuna faida ukilinganisha na kuishi eneo la square mita 1000 lisilo rasmi,” amesema Mhe. Silaa.
Amewataka wananchi wanaorasimishiwa maeneo yao kutekeleza
dhana ya kujitolea wakati wa zoezi hilo kwa kuwa, ndiyo dhana ya ujamaa na
falsafa ya Tanzania inayomfanya mwananchi kuelewa sehemu ya eneo lake imetolewa
kwa ajili ya matumizi ya huduma kama vile barabara, makaburi na shule.
Amebainisha kuwa, utekelezaji huo ukifanyika basi uvamizi
kwenye maeneo ya wazi unaofanyika sasa kwenye maeneo mbalimbali utapungua.
"Tunapopanga na kupima maeneo, mtu anapopata kiwanja chake
basi ajue nina kiwanja eneo fulani lakini kuna maeneo ya umma ambayo yapo na
wakati mimi napata kiwanja nimeyalipia," amesema Mhe. Silaa.
Kwa mujibu Mhe. Silaa, yapo maelekezo kwa maeneo
yanapopangwa na kupimwa kwamba mtu anaponunua kiwanja chake cha makazi ajue
hawezi kuishi peke yake na atakuwa amelipia pia maeneo ya huduma kama vile ya
kuabudia na kuzikia.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Mhe. Geophrey Pinda amewaeleza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Ardhi Maliasili na Utalii kuwa, Wizara yake imeendelea kutoa elimu hususan
kwenye maeneo yanayomilikishwa kwa hati.
Ametolea mfano wa uwekaji mipango ya matumizi ya ardhi
katika vijiji kuwa, zoezi hilo limekuwa likihusisha wananchi wa maeneo husika
huku akiweka wazi kuwa, elimu imekuwa ikitolewa kwa makundi mbalimbali ili
kujua umuhimu na namna ya kutunza hati.
“Ushirikishwaji katika zoezi mipango ya matumizi ya ardhi
kwenye vijiji ni mkumbwa sana maana wanaokwenda kusimama na zoezi ni wananchi
wenyewe kwa hiyo utoaji elimu ni mkubwa na wananchi wanaelimishwa kwa makundi
ili kuelewa hati inayokwenda kutolewa,” amesema.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendesha semina ya siku moja kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii kwa lengo la kuelezea hatua zilizofikiwa kwenye Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Tanzania (LTIP) hadi kufikia Mei 15, 2024.
Mradi huo unatekelezwa kupitia vipengele vinne ambavyo ni kuongeza usalama wa milki za ardhi, kuimarisha mifumo ya taarifa za ardhi (ILMIS), kujenga miundombinu ya ardhi pamoja na kusimamia mradi.
Na. Munir Shemweta
0 Maoni