WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza taarifa maalum ya udhibiti
wa vitendo vya uvuvi haramu iwasilishwe kabla ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi
haijawasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2024/2025.
Ametoa agizo hilo jana katika hafla ya uzinduzi wa boti
maalum kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika bahari hapa
nchini iliyofanyika bandarini jijini Dar es Salaam.
“Taarifa kuhusiana na shughuli maalum ya udhibiti wa vitendo
vya uvuvi haramu katika ukanda wa Bahari kuu iwasilishwe kabla ya Wizara ya
Mifugo na Uvuvi haijawasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2024/2025,” amesema.
Ameishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kushirikiana na
Serikali ya Tanzania katika kufanikisha mipango ya maendeleo ambayo imechangia
dola za Marekani 500,000 kwenye ununuzi wa boti hiyo. “Ninaiomba Serikali ya
Japan isichoke kutusaidia ili tuweze kukamilisha utekelezaji wa mikakati
iliyopo katika eneo hili la kukabiliana na uhalifu nchini,” amesema.
Vilevile, amelishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP) kwa kuchangia dola za Marekani 400,000 kwenye mradi huo.
“Mchango wenu tunauthamini sana, wakati wote mmekuwa mkishirikiana nasi katika
maeneo mengi, kwa niaba ya wananchi na Serikali ya Tanzania ninawashukuru
sana,” amesema.
Mapema, akitoa
taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga alieleza kuwa ununuzi wa boti hiyo
ni sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa Mradi wa Kukabiliana na Vitendo vya
Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu unaotekelezwa na Serikali.
Alisema mapambano hayo yatahusisha kuimarisha juhudi za
kukabiliana na vitendo vya kihalifu kama vile uvuvi haramu, uhamiaji haramu,
uharamia, usafirishaji wa dawa za kulevya na utoroshwaji wa nyara za Serikali.
Akieleza sifa za boti hiyo alisema: “Ni boti ni mpya, ya
kisasa yenye uwezo mkubwa wa kuhimili utekelezaji wa majukumu ya doria. Boti
hii ya doria imepewa jina la Patrol Boat Sailfish (PB Sailfish).”
Amesema uwepo wa boti hiyo utaleta mageuzi makubwa kwenye
ulinzi na usalama wa baharini kwani itawezesha kufanya doria na kaguzi kwenye
maji ya Tanzania. “Itafanya utafutaji na uokozi pindi zikitokea ajali baharini
na kuimarisha ulinzi kwenye pwani yetu kwa kuwa imewekewa mitambo maalum ya
silaha pamoja na mtambo maalum wa kuzima moto… boti hii ni mwarobaini wa
kuhakikisha pwani ya Tanzania iko salama.”
Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini, Yasushi Misawa
amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika
mapambano hayo na kueleza umuhimu wa mradi kuwa utaimarisha uwezo wa Tanzania
wa kuzuia shughuli haramu ndani ya bahari ya Tanzania.
Alitumia fursa hiyo kueleza kuwa nchi yake itaendelea kuimarisha mahusiano wa kirafiki uliopo baina ya nchi hizo mbili kwa zaidi ya miaka 60 tangu uhuru wa Tanzania. “Kwa mtazamo wa usafiri wa majini, JICA imeamua kutoa fedha zaidi kwa ajili ya mradi wa ukaratbati wa bandari ya Kigoma. Japan pia kwa muda mrefu imekuwa ikiisaidia Tanzania katika kukuza sekta ya uvuvi,” alisema Balozi Misawa.
Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameishukuru
Serikali kwa kupatikana kwa boti ya doria kwenye bahari na maziwa makuu kwa
sababu itatatua changamoto ya uhalifu.
Ameishukuru Serikali kwa kupambana na milipuko baharini
pamoja na kuwakabili wahusika wa vilipuzi ambapo hadi sasa watuhumiwa wapatao
24 wamekwishakamatwa. “Kati ya hao, 13 ni wasambazaji wa vilipuzi, 10 ni wavuvi
na mmoja ni mfadhili wao,” alisema.
Amesema jitihada zinazafanyika kudhibiti vitendo hivyo
katika maeneo yote ya ukanda wa bahari ya Hindi na baadaye nguvu zitaelekezwa
kwenye maziwa makuu.
Akitoa taarifa kuhusu ufanisi boti hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Hosea Ndagala alisema boti hiyo ina uwezo kukimbia kwa kasi ya km. 47 kwa saa (nautical miles 25), inaweza kubeba wahalifu 20 kwa pamoja, inaweza kutumika kubebea wagonjwa (ambulance), kuzima moto na kwenye shughuli za uokoaji.
0 Maoni