Ni hivi --- hii ilikuwa ni safari ya majaribio na ilipangwa
kutumia saa 4 au muda wowote zaidi kidogo kutokana na mahitaji ya majaribio.
Nini maana ya safari hii?
Kuna vitu vingi vya kupima, mfano: mfumo wa umeme, mfumo wa
usalama, mfumo wa Tehama, kamera za njia nzima, uwezo wa injini kufanya mambo
kadha wa kadha, uwezo wa mabehewa, utaalam wa waendeshaji na wasimamizi waliopo
kituoni Dar, joto la magurudumu baada ya msuguano na reli ambapo taarifa
hutumwa kupitia mfumo wa kielektronikia, n.k.
Kwa hiyo muda wa saa 4 ulikuwa ni wa kujaribu tu. Hata
hivyo, tuliondoka saa 8:52 mchana na kufika saa 12:55 usiku. Ni saa 4 ingawa
kila mtu aliyefuatilia ana namba zake lakini wote tunaishia hapo hapo ---
takriban saa 4.
Safari hii ilifuta ratiba za kusimama njiani (Ngerengere na
Morogoro) baada ya kuchelewa kuondoka kutokana na shughuli iliyotangulia
stesheni pale lakini iliheshimu kanuni za kupunguza mwendo kwa kuwa ni
majaribio.
Umbali wa Dar hadi Morogoro ni km 205 za reli hii na hadi
Makutupora ni km 336 lakini hii imeishia Mkonze jijini Dodoma. Maana yake
safari hii haikufikia umbali huo.
Umbali wa barabara Dar- Dodoma ni km 450.
Kupima mwendo kasi hivi sasa ni kazi bure tu kwa sababu
uwezo wa treni hii unazidi km 200 kwa saa lakini kwa muundo wa reli yetu
inapangwa iwe km 160 kwa saa kwa treni ya abiria. Treni ya mizigo itakwenda km
120 kwa saa.
Aidha, itakapoanza safari itakuwa ikitumia saa 3 labda na
dakika chache hivi kutoka Dar hadi Dodoma ikijumuisha kusimama kwa dk 5 katika
vituo vidogo na dk 10 katika vituo vikubwa. Tusisahau na jukumu la kupunguza
mwendo (deceleration) kabla ya kusimama au wakati wa kuondoka kwa kuanza
taratibu na kuongeza (acceleration).
Treni hii ni ya kisasa na mambo yote yanafanywa
kielektronikia.
Kufikiri kwamba eti tumedanganywa kuhusu mwendo kasi wake ni
akili za kitoto. Halafu iweje? Serikali au TRC itapata nini hapo? Kisha?
Tusubiri safari rasmi zianze ndiyo tutoe maoni kuhusu
mwendokasi.
Nilitahadharisha Jumamosi kuhusu fikra hizi nilipoongea na
waandishi wa habari.
Mobhare Matinyi
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali.
0 Maoni