Wazee wa wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza wamewataka watanzania kuendelea kudumisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuendelea kuyaenzi mambo mema waliyotaka waasisi wa muungano huo uliotimiza miaka 60 hii leo.
Mwenyekiti wa Baraza la uUhauri la Wazee wilaya ya Ilemela Yusuph Mzee amesema mshikamano ulioanzishwa miaka 60 iliyopita ni vyema ukaendelezwa kwa kufanya mambo mema ya kujenga nchi na kuepuka machafuko.
“Wazee wetu waliounganisha nchi hii Tanganyika na Zanzibar na kuwa Tanzania tuendelee kudumisha amani iliyowekwa na wazee wetu na kuishukuru serikali ya sasa kwa kuendelea kuidumisha na kuilinda amani hasa pale maadui walipotaka kuiharibu amani ya nchi hii,” alisema Mzee.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Ilemela akawataka kushikamana katika kudumisha muungano bila kujali itikadi za vyama ili nchi iweze kusonga mbele.
“Natambua na kuelewa Tanzania ya sasa inaongozwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa lakini vinaongozwa na Chama cha Mapinduzi hivyo katika kuuenzi muungano tusiangalie tofauti za vyama vyetu bali tushikamane letu liwe moja,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala wa mkoa huo Balandya Elikana akaeleza manufaa ya muungano ikwemo na kukua na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, uwekezaji kwenye sekta ya usafiri wa majini na anga pamoja na kudumisha amani.
“Muungano wa leo unadumu sababu ya wazee wetu waliozaliwa kabla ya huu muungano wameendelea kuudumisha vizuri hivyo na sisi tuuendeleze tusikubali kuishi njiani na huu muungano una manufaa mengi sana unaendelea undugu wetu wa damu leo hii kuna Wazanzibari wengi sana wanaishi huku bara na kule Zanzibar wapo watu wa huku bara huo ndiyo undugu wa kweli tuudumishe fursa mbalimbali za kiuchumi tena zimeongezeka kwahiyo unaona ni kwa jinsi gani muungano huu umekuwa wa manufaa kwetu,” alisema Elikana.
Leo ni miaka 60 tangu Tanganyika na Zanzibar zilipoungana na kuunda nchi ya Tanzania na maadhimisho ya mwaka huu yanaenda na kauli mbiu isemayo miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tumeshikamana na Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa.
0 Maoni