Wanawake nchini wameendelea kupata fursa za uongozi katika
ngazi mbalimbali huku takwimu zikionesha ongezeko la Wanawake katika uongozi
ikiwemo Mawaziri Wanawake kutoka asilimia 15 kwa mwaka 2005 hadi asilimia 37
kwa mwaka 2023. Aidha, Wabunge wanawake wameongezeka kutoka asilimia 22 hadi
kufikia asilimia 37 kwa mwaka 2023.
Hayo yamebainishwa wakati wa uzinduzi wa mradi wa “Think
Equal Lead Smart” wenye lengo la kuhamasisha wanawake na vijana kushiriki
katika nafasi za uongozi na maamuzi uliofanyika Jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza katika uzinduzi huo Naibu Waziri wa Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema takwimu
zinaonesha pia Wanawake Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar
wameongezeka kwa asilimia 38, Madiwani asilimia 29.9. Mabalozi asilimia 25,
Makatibu Wakuu asilimia 22, Manaibu Makatibu Wakuu asilimia 28, Wakuu wa Mikoa
asilimia 31, Makatibu Tawala asilimia 26, Wakuu wa Wilaya asilimia 33 na
Wakurugenzi asilimia 28.
Naibu Waziri Mwanaidi amesema Tanzania imeendelea kutambua
umuhimu wa Wanawake kwa kuwapatia fursa katika nafasi za Uongozi na Maamuzi na
kuongeza ushiriki wao katika ngazi mbalimbali za Uwakilishi, Uongozi na ngazi
za maamuzi. Mabadiliko haya yanatokana na dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Dkt.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha
kuna usawa kati ya Wanaume na Wanawake na katika nyanja zote.
Ameongeza kuwa Wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo
ya familia na Taifa kwa ujumla, hasa ikizingatiwa kuwa kundi kubwa la watu
nchini ni Wanawake ingawa bado wanawake wanakabiliwa na changamoto
zinazowaathiri na kukwamisha maendeleo yao; miongoni mwa changamoto hizo ni
pamoja na uwepo wa mila na destruri zenye madhara, kutopatiwa fursa ya kupata
elimu pamoja na kutoshirikishwa katika shughuli za ujasiriamali na uzalishaji
mali.
"Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa mikataba
ya Kikanda na Kimataifa inayolenga kukuza Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji
Wanawake hapa nchini. Mikataba hiyo imekuwa chachu kwa maendeleo ya Wanawake
ambapo kupitia Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa, nchi yetu inatekeleza afua
mbalimbali zinazochochea Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake
Kiuchumi." amesisitiza Naibu Waziri Mwanaidi.
Aidha, Naibu Waziri Mwanaidi amesema Serikali inatambua
mchango wa Mradi huo unaolenga kuwezesha ushiriki wa wanawake na fursa sawa za
uongozi katika ngazi zote za maamuzi nchini Tanzania na ameahidi kuendelea
kushirikiana Taasisi hiyo kuwafikia Wanawake hasa walio maneno ya pembezoni mwa
nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya CEO
Roundtable of Tanzania Santina Benson amesema Taasisi hiyo imeanzisha mradi huo
kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha Wanawake
wanaoata fursa sawa katika nyanja mbalimbali ikiwemo uongozi katika ngazi za
maamuzi na fursa za kiuchumi.
"Mradi wa Think Equal Lead Smart (TELS) unaosimamiwa na Taasisi yetu unalenga kuwezesha ushiriki wa wanawake na fursa sawa za uongozi katika ngazi zote za maamuzi nchini Tanzania. Hivyo tunaomba Ushirikiano kutoka kwa Serikali na Taasisi nyingine ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huu kwa pamoja" ameeleza Santina.
Na. WMJJWM- Dar es Salaam
0 Maoni