Uwanja wa ndege Sumbawanga ukamilike kwa wakati- Nchimbi

 

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ameigiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga unakamilika ifikapo Machi mwakani na kwa ubora unaotakiwa.

"Niwatake TANROADS kuhakikisha mikataba inazingatiwa, kama ujenzi ni miezi 18 iwe 18 na sio kupitiliza, mfano hapa mmenieleza mmefikia asilimia 8% ujenzi wa ukarabati na upanuzi wa uwanja huu wa ndege wa Sumbawanga badala ya kuwa asilimia 15%,...tunataka kazi hizi zifanyike kwa haraka na ubora," alisema Dkt. Nchimbi.

Dkt. Nchimbi ameitoa kauli hiyo leo mkoani Rukwa wakati akiwaongoza viongozi wa chama na serikali kukagua maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga wakati wa ziara yake mkoani humo hii leo.

Ujenzi wa  uwanja huo utakaogharimu  zaidi ya shilingi bilioni 60 utakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 150, 000 kwa mwaka na utarahisisha zaidi usafiri kwa wakazi na wageni.  Mradi wa ujenzi huo umetoa ajira kwa watu 120 ambapo wazawa ni 114.

Dkt. Nchimbi aliambatana na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla pamoja na Katibu wa Oganaizesheni, Issa Haji Gavu ameanza ziara ya kikazi ya siku kumi katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Ruvuma.

Lengo la ziara hiyo ni kuhuisha uhai wa chama, kutatua kero za wananchi, kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.

Baada ya kumaliza ziara yake katika mikoa ya Katavi, Rukwa na Songwe kwa mafanikio, ziara hiyo ya siku 10, itaendelea kesho katika Mkoa Mbeya na hatimaye katika mikoa ya Njombe na Ruvuma.



Chapisha Maoni

0 Maoni