Wataalamu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na
wenzao kutoka nchini India wakimfanyia mgonjwa upasuaji kwa njia ya tundu dogo
wa kutumia kifaa maalumu (Stent) wa kurekebisha mshipa wa damu uliotanuka sehemu
ya kifua. Wagonjwa watano watafanyiwa upasuaji huo ambao kwa mara ya kwanza
umefanyika hapa nchini kwa kutumia mtambo wa Cathlab.
Kwa mara ya kwanza wataamu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete (JKCI) wamefanya upasuaji kwa njia ya tundu dogo wa kurekebisha mishipa
ya damu iliyotanuka na kupasuka sehemu ya kifua na tumbo kwa wagonjwa watano
wenye matatizo hayo.
Akizungumza leo jijini
Dar es Salaam na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema wagonjwa wenye matatizo hayo
wengi wao walikuwa wakipoteza maisha na wale ambao walikuwa wanapona walipewa
rufaa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Dkt. Kisenge alisema upasuaji huo umefanywa na madaktari
wazawa kwa kushirikiana na madaktari kutoka India na tayari mgonjwa mmoja alishafanyiwa upasuaji huku wengine
watatu watafanyiwa upasuaji huo leo na
mmoja kesho.
"Kwa mara ya tatu
tunavunja rekodi tumefanya matibabu makubwa ya kurekebisha mishipa ya damu
ambayo imetanuka na kupasuka hii ni tatizo ambalo watu wengi wanalipata na
kupoteza maisha ghafla na wanaobaki tunawapeleka nje ya nchi lakini hivi sasa tutaanza kuwahudumia hapa nchini.”
"Ni upasuaji
mkubwa kufanyika Tanzania na Afrika Mashariki na Kati tumevunja rekodi
tunampongeza Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapenda wananchi
wake na kutoa kiasi cha shilingi milioni 900 za matibabu ya kibingwa katika
Taasisi yetu," alisema Dkt. Kisenge.
Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo alisema mishipa ya damu
ya tumboni na kifuani kutanuka na kupasuka kunasabahishwa na vitu vingi ikiwemo
shinikizo la juu la damu ambayo
haitibiwi vizuri,uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe uliokithiri na uzito
mkubwa.
Dkt. Kisenge alisema katika Taasisi hiyo kuna wagonjwa
wapatao 30 wanaosubiri kupata matibabu hayo ambapo gharama zake ni shilingi
milioni 80 endapo mgonjwa atatibiwa hapa nchini na milioni 150 akitibiwa nje
ya nchi.
"Tutaendelea kutoa matibabu haya na tutaendelea kuwa na
matibabu mapya mengine kwani wataalamu wetu wanajifunza kila siku. Upasuaji huu
tulioufanya ukifanyika kwa njia ya kufungua kifua unachukua saa nane ila kwa
njia ya tundu dogo ni saa mbili hii ni njia nzuri japo gharama ni kubwa ila
Mhe. Rais wetu ametoa fedha ili wananchi wasaidiwe,” alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa
ya damu kutoka nchini India Gireesh Warawdekar alisema upasuaji huo unaenda
sambamba na mafunzo wanayoyatoa kwa wataalamu wa JKCI ili nao waweze
kuwahudumia wananchi wenye shida za mishipa ya tumbo na kifua.
“Aina hii ya upasuaji ambao tunaufanya kwa njia ya tundu dogo
kwa kutumia mtambo wa Cathlab ni upasuaji mgumu lakini ni mzuri kwani hautumii
muda mwingi kuufanya pia mgonjwa anayetibiwa anakaa muda mfupi hospitali na
hapiti katika kipindi kigumu cha maumivu kama ilivyo kwa upasuaji wa kufungua
kifua,”alisema Dkt. Warawdekar.
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema walikuwa hawana utaalamu wala vifaa vya
kuwezesha kufanyika kwa upasuaji huo lakini kwa uwekezaji uliofanywa na Mhe.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wameweza kufanikisha hilo.
"Wataalmu hawa wa kutoka nchini India wapo na ujuzi
mkubwa ambao wanatufundisha sisi,
tunatumia mashine zetu wao wamekuja na kifaa chenye gharama kubwa
kinachotengenezwa ambacho kinatumika katika upasuaji, nasi tunaelekea huko
kutengeneza wataalamu watakaofanya upasuaji wa aina hii,”alisema Dkt. Angela.
Naye Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya
damu wa JKCI Alex Joseph alishukuru ujio
wa madaktari hao kutoka nchini India kwani wamefanikiwa kumfanyia upasuaji mzee
wa miaka 66.
"Tulichukua saa mbili kufanyia upasuaji tulifanikiwa kwa
kumuwekea kifaa maalumu (Stent) sasa hivi mgonjwa yuko vizuri ameamka na
anaweza kutembea kesho anarudi kwake na upasuji wa awali wa kupasua tumbo na
kifua ulikuwa na hatari kubwa ya kifo ila huu wa sasa ni salama zaidi,” alisema
Dkt. Alex.
Mmoja wa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji huo kutoka Zanzibar
Ali Suleiman alisema alipata matatizo ya moyo na baada ya uchunguzi katika
Hospitali ya Mnazi mmoja alibainika kuwa na matatizo ya mishipa ya damu na
kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.
"Nimefika hapa Januari 1,2024 kulikuwa na changamoto
nyingi hadi leo nimefanyiwa upasuaji, ni
upasuaji mzuri kwangu nawashukuru sana madaktari wote walionifanyia upasuaji
kwa usalama najisiki nina nguvu na naweza kutembea kwa miguu.”
Ninawasihi wenzangu wenye matatizo kama haya wasihangaike
kwenda kutibiwa nje ya nchi waje hapa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) watatibiwa mimi nimefanyiwa upasuaji jana usiku na kama unavyoniona niko
vizuri tofauti na kabla sijafanyiwa,”alisema Mzee Suleiman.
Wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji ni wale wenye shida za mishipa
ya damu kutanuka, kupasuka kwa mishipa ya damu na kuziba kwa mishipa (Aortic
Aneurysm, Dissection, Peripheral artery disease).
0 Maoni