Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) inaendelea
kuwachukulia hatua wale wote watakaojihusisha na unajangili wa mazao ya misitu
kwa kuwafikisha mahakamani kwa mujibu wa Sheria.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) wakati akijibu Swali la Mhe. Aleksia Asia Kamguna (Mb)
ambaye alitaka kujua mikakati ya Serikali ya kupanda miti katika Mkoa wa
Morogoro hususan Milima ya Uluguru na kandokando ya Mto Fulua, Mnyera na
Kilombero.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii
kupitia Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na
Halmashauri na Wadau mabalimbali imepanda jumla ya miti 9,026,605 (ikiwemo miti
1,000,000 ya mikarafuu kwa ajili ya viungo) katika mpaka wa msitu, vijiji
vinavyopakana na msitu wa Uluguru mkoani
wa Morogoro.
Aidha, Mhe. Kitandula aliongeza kuwa katika kuhakikisha
uhifadhi unaendelezwa katika Milima ya Uluguru, zoezi la kupanda miti
lilifanyika kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024.
Pia, Mhe. Kitandula alisema kuwa kwa upande wa maeneo ya Mto
Fulua, Mnyera na Kilombero, Wizara inaendelea na jitihada za kutunza maeneo
hayo kwa kupanda miti rafiki wa maji pamoja na kuendelea kutoa elimu ya umuhimu
wa uhifadhi.
”Katika kuimarisha jitihada hizo Wizara inashirikiana na
taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali kuelimisha jamii,
kuwezesha jamii kubuni na kuanzisha vyanzo mbadala vya kujipatia kipato na
kupanda miti stahili katika maeneo ya kingo za mito. Wadau hao ni pamoja na
Mfuko wa Uhifadhi Misitu Tao La Mashariki, AGRIWEZESHA, WWF, AWF, SAGOT, TAF na
Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA),”alisema Mhe. Kitandula.
Na. Anangisye Mwateba-Bungeni Dodoma
0 Maoni