Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania
kuepuka matumizi ya Dawa za Kulevya kwani yanaharibu nguvukazi ya Taifa hasa
vijana ambao wanategemewa kuongoza kufanya shughuli za uzailishaji na
kuharakisha maendeleo.
Ametoa wito huo leo (Jumanne Aprili 2, 2024) katika sherehe
za uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika kitaifa Katika Viwanja vya
Chuo cha Ushirika Moshi Mkoani Kilimanjaro.
“Idadi kubwa ya waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya ni
watoto na vijana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 24. Kundi hili ni nguvukazi
ya Taifa letu, Serikali, haiwezi kunyamaza itaendelea kufanya msako mkali ili
wahusika wote wa biashara hiyo haramu wachukuliwa hatua kali,” amesema Majaliwa.
Amesema kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu wa udhibiti wa
biashara ya dawa ya kulevya imeendelea kuongeza kasi ya mapambano ili kukomesha
biashara, kilimo na matumizi ya dawa za kulevya. “Hatua kali zitachukuliwa
dhidi ya wote wanaojihusisha na kilimo hicho haramu pamoja na biashara ya dawa
za kulevya.”
"Viashiria vya kuwepo kwa ongezeko la matumizi ya dawa
za kulevya nchini ni pamoja na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watumiaji
wanaotafuta matibabu, kuongezeka kwa watu wanaokamatwa wakitumia dawa za
kulevya, kiasi cha dawa za kulevya zinazokamatwa zikiingizwa nchini na kuwepo
kwa uhalifu unaohusishwa na matumizi ya dawa za kulevya hasa uporaji, wizi na
ukabaji."
Amesema mbio za mwenge wa uhuru za mwaka 2024 zitaendelea
kutoa hamasa kwa jamii kusitisha kilimo haramu cha bangi, biashara na matumizi
ya dawa za kulevya. Aidha, utajiekeleza kwenye kuhamasisha jamii kulima kilimo
cha mazao halali ya biashara na chakula, pamoja na kuhamasisha jamii kushiriki
katika shughuli nyingine halali na zenye staha.
"Hivi karibuni, kumeibuka aina nyingine ya bangi yenye
kiasi kikubwa cha kilevi ikifahamika kama “skanka”. Aina hii ya bangi yenye
sumu nyingi huchanganywa kwenye sigara na vijana wamekuwa wakitumia skanka
ambayo imekuwa ikipelekea kuchanganyikiwa," amesema Majaliwa.
Amesema kuwa vijana wamekuwa wakitumia bidhaa hizo wakifahamu
uwepo wa skanka na wengine bila kufahamu na hujikuta wanakuwa waraibu wa bangi.
Amesema Idadi kubwa ya waathirika wa matumizi ya dawa za
kulevya ni watoto na vijana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 24.
Kundi hili ni nguvukazi ya Taifa letu ambayo
inategemewa kuongoza kufanya shughuli za uzailishaji na kuharakisha maendeleo
ya Taifa, amesema Majaliwa.
Amesema Serikali, itaendelea kufanya msako mkali ili wahusika wote wa biashara hiyo haramu wachukuliwe hatua kali, na kuongeza kasi ya mapambano ili kukomesha biashara, kilimo na matumizi ya dawa za kulevya.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amesema mbio za
Mwenge wa Uhuru mwaka huu utaendelea
kuhimiza mapambano dhidi ya Rushwa, huku akitoa wito kwa Watanzania
kupambana na vitendo vya rushwa.
"Tafiti za taasisi za kitaifa na kimataifa zinaonesha
kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa. Kwa
mujibu wa taarifa ya utafiti wa REPOA iliyotolewa Machi 9, 2022 Tanzania
inafanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa ambapo zaidi ya asilima 77 ya
Watanzania waliohojiwa walikiri kuwa rushwa imepungua nchini."
Kadhalika, amesema Serikali kupitia mbio za mwenge itaendelea
kuwashurikisha wananchi na wadau wengine katika mapambano dhidi ya maambukizi
ya mapya ya virusi vya UKIMWI.
"Watanzania wenzangu ninaomba mfahamu kuwa, afya zetu
ndio mtaji wetu. Hatuwezi kufikia ndoto zetu tulizojiwekea kimaisha bila kuwa
na afya njema, hivyo wananchi wote tushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi
ya UKIMWI."
Naye, Waziri wa Habari, Vijana Utanaduni na Michezo wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Tabia Mwita Maulid, Amesema mbio
za mwenge wa Uhuru zimeendelea kudumisha Uhuru, amani mshikamano uzalendo na
umoja wa kitaifa pia zimekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kijamii.
Awali, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana
ajira na wenye Ulemavu, Mheshimiwa Patrobas Katambi amesema falsafa ya Mwenge
wa Uhuru imekuwa ni kuwaunganisha watanzania, kuleta matumaini pamoja na
kukagua miradi inayotoa huduma kwa wananchi ili kusogeza huduma kwa wananchi.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni