Tembo waongezeka Matokeo ya Sensa ya Wanyamapori

 

Waziri  wa  Maliasili  na  Utalii  Mhe. Angellah  Kairuki  ametangaza rasmi matokeo ya sensa  ya wanyamapori  katika  mifumo  mitatu ya ikolojia  ya Nyerere-Selous-Mikumi, Saadani-Wamimbiki na Serengeti ambayo ni miongoni mwa mifumo  11  ya ikolojia  nchini.

Akitangaza matokeo hayo katika mkutano wa wadau wa uhifadhi na utalii uliofanyika jijini Arusha, Mhe. Kairuki amesema, sensa katika mfumo  ikolojia wa Nyerere-Selous-Mikumi, unaonesha kuimarika kwa  spishi 22 za wanyamapori wakiwemo nyati/buffaloes (59,878), tembo/elephants (20,006), nyumbu/wildebeest 19,060, kongoni/hartebeest (18,361), swalapala/impala (14,031), ngiri (13,806) na idadi ya Wanyama walioonekana kwa idadi ndogo ni twiga/giraffe (1,679), Tandala mkubwa/greater kudu (1,414) na puku/sheshe (496).

"Katika mfumo huu  kumekuwa na ongezeko la tembo  20,006 (2022) ikilinganishwa na sensa ya awali  15,501 (2018) na Viashiria vya ujangili wa tembo au vifo vya tembo vimepungua kwa kiasi kikubwa  kutoka 16% mwaka  2018 hadi  hadi 0.8% mwaka 2022," ameeleza Mhe. Kairuki.

Mhe. Kairuki ameitaka Idara ya Wanyamapori  Wizara ya Maliasili  na  Utalii kuchukua hatua  za haraka  kulinda idadi ya Sheshe/puku ambao wanapatikana Tanzania  pekee  waliosalia katika maeneo yao ya asili yakiwemo mapori ya akiba ya Kilombero na ziwa Rukwa ambao idadi  yao imepungua kwa kiasi kikubwa kutoka  (1,579 mwaka 2018) hadi  (496 mwaka 2022).

Vilevile, uhesabuji wa Nyumbu katika mfumo ikolojia wa Serengeti matokeo ya sensa hii yamebaini uwepo wa nyumbu wanapatao 1,597,850. Idadi hii inaonyesha kuimarika kwa nyumbu ikilinganishwa na sensa ya hapo awali (2015) iliyoonyesha uwepo wa nyumbu wapatao 1,326,709.

Kwa upande wa mfumo ikolojia  wa Saadani - Wami - Mbiki Matokeo ya sensa  yameonesha uwepo wa wanyamapori wachache  unahusishwa na hali ya upya wa hifadhi hizi ambapo hapo awali,hifadhi ya Saadani ilikuwa pori tengefu na sehemu nyingine ilikuwa shamba la mifugo na zoezi la kuongeza wanyamapori lilifanyika miaka ya hivi karibuni .

Aidha , Mhe. Kairuki  amesema   kwa mwaka wa fedha  2024-2025 wizara imeweka mikakati ya kufanya sensa ya wanyamapori  katika mifumo  yote ya ikolojia kwa lengo la kuimarisha uhifadhi  na kukuza kuwa na utalii endelevu  ambapo ametoa rai  kwa wadau  kuonga mkono jitihada hizi za Serekali  katika kuhifadhi  utajiri  wa Maliasili  ya  Wanyamapori .

Chapisha Maoni

0 Maoni