Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ina lengo
la kuhakikisha barabara zote nchini zinapitika kwa asilimia 85 ili kuinua
uchumi na kuwezesha huduma za kijamii kwa wananchi ifikapo mwaka 2025/2026.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor
Seff wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TARURA
kilichofanyika mkoani Morogoro leo tarehe 4 Aprili, 2024.
Mhandisi Seff amesema Baraza hilo ambalo lipo kisheria ni njia
ya kuwashirikisha wafanyakazi ili kutoa michango yao ikiwemo masuala mbalimbali
kuhusiana na utendaji wa Wakala.
Mhandisi Seff amesema kwa sasa zaidi ya Km 100,000 ya Mtandao
wa Barabara za Wilaya ni za udongo na zinaathirika zaidi wakati wa mvua zinaponyesha
hivyo lengo lao ni kuwezesha barabara hizo ziweze kupitika msimu wote.
“Mtandao wetu wa barabara za Wilaya una urefu wa Km
144,429.77, lengo letu ni kuhakikisha barabara zote zinapitika msimu wote kwa
asilimia 85 ifikapo mwaka 2025/2026," amesema Mhandisi Seff.
Pia ameongeza kuwa vikao hivyo vinasaidia kuboresha maslahi
ya wafanyakazi na namna ya kuweza kuboresha utendaji kazi wa TARURA kutokana na
maoni na mapendekezo yao.
Naye, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi Serikali za
Mitaa Tanzania (TALGWU) Dkt. Almas Suleiman amewapongeza TARURA kwa kurudisha
mawasiliano ya barabara katika msimu wa mvua na kuwakumbusha Watendaji wa
TARURA kuisikiliza jamii ili kuepuka migogoro inayoweza kutokea katika maeneo
yao.
Wakati huo huo Mwakilishi kutoka Chama cha Wafanyakazi wa
Migodi, Nishati na Ujenzi (TAMICO) Bw. Paternus Rwechungura ameipongeza TARURA
kwa kufanya kikao hicho na kuwaomba wajumbe kujiunga na chama hicho ili kuweza
kuwasaidia wafanyakazi mara wapatapo changamoto za kikazi.
Bi. Tulia Msemwa Mwakilishi
wa Kamishna wa Kazi, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye
Ulemavu, amesema wao kama wasimamizi wakuu wa vyama vya wafanyakazi mahali pa
kazi awewaasa wajumbe kuweza kuchangia maoni na mapendekezo ambayo yatasaidia
Wakala kufikia malengo na dhima kwa yale waliyojiwekea ili kuleta ufanisi
kulingana na dira ya Wakala hiyo.
0 Maoni