Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeendelea
kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa kujenga barabara, vivuko na
madaraja katika maeneo mbalimbali mkoani Rukwa ili kuinua shughuli za kijamii
na kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa TARURA Mkoa wa
Rukwa, Mhandisi William Lameck alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya
kazi kubwa katika kuimarisha miundombinu ya barabara za wilaya nchini.
Mhandisi Lameck amemshukuru Rais Samia kwa kuongeza bajeti
ya TARURA Mkoa wa Rukwa kutoka Shilingi Bilioni 5.63 hadi kufikia Shilingi
Bilioni 12.3 ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuimarisha mtandao wa barabara
mkoani humo.
“Barabara kwa kiwango cha changarawe zimeongezeka kutoka Km
867.25 hadi Km 1,143.05," alibainisha.
“Tumeongeza mtandao wa barabara za lami na kufanyia
matengenezo ya kawaida maeneo korofi jumla ya Km 196.66, ujenzi wa lami Km 0.8
na zege Km 1.55 zitatengenezwa katika Manispaa ya Sumbawanga na Wilaya ya
Kalambo na Nkasi," alisema.
"Pia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe Km 179.5 na ujenzi wa
daraja la Kavunja lenye urefu wa mita 39 linalounganisha vijiji vya Kirando,
Kazovu na Korongwe wilayani Nkasi lenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.76 ambapo
ujenzi wake umekamilika na daraja linatumika.
Amesisitiza daraja hilo limepunguza gharama za usafiri na
usafirishaji ambapo hapo awali wananchi walikuwa wanazunguka katika vijiji vya
Wilaya ya Kalambo lakini sasa wanatumia daraja hilo bila kuwa na wasiwasi juu
ya mali zao na usalama wao.
Mkazi wa Nkasi Bi. Sarafina Mbalamwezi ameipongeza kwa kile
inachokifanya kuhakikisha miradi ya barabara inatekelezwa na kukamilika kwa
wakati na wananchi kuondokana na changamoto ya barabara.
Alisema uboreshaji wa miundombinu ya barabara umeweza
kuwasaidia wananchi kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta
huduma mbalimbali ikiwemo ya matibabu.
Mkazi wa Sopa wilayani Kalambo, Bw. Amon Kabwe amemshukuru
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kuboresha miundombinu vijijini
ili kuhakikisha wananchi wanasafiri na kusafirisha mazao yao sokoni kwa
urahisi," alisema.
Alisema hapo awali kulikuwa na changamoto ya barabara
kutopitika hasa kipindi cha masika lakini kwa sasa barabara hizo zinapitika
muda wote na madaraja korofi yametengenezwa na yote yanatumika.
0 Maoni