Tanzania yaongoza kwa idadi kubwa ya Simba, Chui na Nyati barani Afrika

 

Tanzania inaendelea  kujivunia kuwa na utajiri mkubwa wa Rasilimali ya  Wanyamapori ambapo  inashikilia nafasi ya kwanza barani Afrika  kwa kuwa na idadi  kubwa ya Simba, Chui na Nyati.

Haya yalibainishwa na Mkurugenzi  Mkuu  wa  Taasisi  ya  Utafiti  wa  Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dkt. Eblate  Ernest  Mjingo  katika hafla ya uzinduzi wa matokeo ya sensa ya wanyamapori katika  mifumo ikolojia mitatu ya  Nyerere-Selous-Mikumi, Saadani-Wamimbiki na Serengeti.

Dkt. Mjingo alieleza kuwa, kwa mujibu wa taarifa ya Umoja  wa Kimataifa wa Uhifadhi na Kulinda Ualisia (IUCN) ya mwaka 2023, Tanzania inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya simba  barani Afrika, ambapo ina jumla ya  simba 17,000 ikifuatiwa na Afrika  Kusini yenye simba 3,300 na Botswana  yenye Simba 3,064.

Vilevile, kwa  upande wa  nyati Tanzania inashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na nyati 225,000, ikifuatiwa na Afrika  Kusini yenye nyati 46,000 na ya tatu ni Msumbiji  yenye nyati 45,000.

Kwa upande wa chui Tanzania inaendelea  kushika rekodi ya kwanza kwa kuwa na idadi ya chui  24,000 sambamba na kushika nafasi ya tatu kwa kuwa na tembo  60,000.

Aidha, Dkt. Mjingo amebainisha hali ya ustawi wa uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini ni kutokana na juhudi kubwa za Serikali  katika kuhifadhi ambapo imeendelea kuwezesha tafiti mbalimbali kufanyika pamoja na sensa za wanyamapori sambamba na  mchango  mkubwa wa usimamizi na ulinzi shirikishi  wa Mamlaka  za Uhifadhi za TANAPA,  TAWA  na  Ngorongoro.



Chapisha Maoni

0 Maoni