WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amesema Serikali inaendelea na
uratibu wa uanzishaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika na tayari sh. bilioni 15.7
zimekusanywa kutoka kwa wanahisa.
Amesema kiasi hicho ni sawa na asilimia 78.5 ya mtaji wa sh.
bilioni 20 zinazohitajika na kwamba kuanzishwa kwa benki hiyo, kutaviwezesha
vyama vya ushirika kupata mikopo yenye riba nafuu na kuendesha shughuli zake
kwa tija.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 17, 2024) wakati
akizungumza na wadau wa Kongamano la Kumi la Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo
na Uvuvi lililofanyika katika ukumbi wa Jenerali Venance Mabeyo, jijini Dodoma.
"Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuchukua hatua
mahsusi za kuimarisha ushirika hapa nchini. Hatua hizo ni pamoja na kufanya
maboresho ya mifumo ya uendeshaji wa vyama vya ushirika ili kuongeza
ufanisi."
Amesema Serikali imefanya maboresho ya kitaasisi kwa lengo
la kuongeza tija na ufanisi kwa kuunganisha Taasisi ya Utafiti wa Chai
Tanzania, Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania, Taasisi ya Utafiti wa Kahawa
Tanzania kuwa sehemu ya muundo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).
Amesema Serikali pia imeunganisha Bodi ya Chai Tanzania na
Umoja wa Wakulima Wadogo wa Chai ili kuwa na Bodi moja. Pia imehamishia
shughuli za Bodi ya Pareto Tanzania kwenda kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka
na Mazao Mchanganyiko.
"Kwa upande wa sekta ya mifugo na uvuvi, Serikali
inaendelea kukamilisha utaratibu wa kuunganisha Bodi ya Nyama na Bodi ya
Maziwa, kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji pamoja
na Mamlaka ya Bidhaa na Miundombinu ya Mifugo."
Amesema maboresho hayo ni sehemu ya jitihada za makusudi za
Serikali ya Awamu ya Sita katika kuongeza ufanisi na kukuza uchumi wa nchi
kupitia sekta hizo. Hivyo, ametoa wito kwa wadau wa kongamano hilo kujadili
namna bora ya kuiwezesha Tanzania kuwa sehemu ya maendeleo ya kilimo smati.
Amesema hivi sasa dunia inaendelea kujadili suala la
mabadiliko ya tabianchi, mifumo ya chakula, akilibandia, hewaukaa pamoja na
masuala mazima ya ubunifu na teknolojia.
"Katika hizi siku tatu za Kongamano, hakikisheni
mnajadili kuhusu masuala hayo na kuja na mapendekezo ya namna ya kuboresha sera
zetu na mifumo yetu katika sekta hizi. Leteni mapendekezo ili twende na wakati,
tuongeze tija, tukuze mitaji na uwekezaji kwenye sekta hizi muhimu katika
uchumi wa nchi."
Mapema, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema katika
kufanya maboresho ya sekta ya kilimo hususan sekta ya uzalishaji mbegu,
Serikali imeanza utaratibu wa kuwawezesha wazalishaji binafsi wa mbegu kwa
kuwatambua na kuwapatia mashamba ili kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za
kilimo.
"Serikali inaendelea na mkakati wa kuona ni namna gani tunaweza kutoa ruzuku kwa wazalishaji wa mbegu ili nchi yetu iweze kujitosheleza katika uzalishaji wa mbegu bora.
0 Maoni