Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amefungua
kikao cha kwanza cha Kamati kuu ya Kuratibu Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima
maarufu kama Nane nane kwa Kanda ya kati ambapo Mwaka huu (2024) zinatarajiwa
kufanyika kitaifa kwenye Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza na wajumbe walioshiriki kikao hicho kwenye
ukumbi wa ofisi yake jengo la Mkapa Jijini Dodoma, Mhe. Senyamule amewataka
washiriki hao kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwenye Jukumu lolote
watakalopangiwa ili kuondoa sintofahamu kuelekea kilele cha siku hiyo.
“Kila mtu ni vema atimize wajibu wake, usingoje hadi uambiwe
nini cha kufanya. Kitu chochote kinachotakiwa kufanyika kifanyike ili
Maadhimisho hayo yaweze kuwa na tija kama inavyotarajiwa na ukizingatia ni
sherehe ya Kitaifa ambayo itajumuisha mambo mengi katika hizo siku kuanzia siku
ya kwanza hadi siku ya mwisho.
“Kila mmoja awe sehemu ya maadalizi ili kuhakikisha lengo
letu linatimia kwa Kiwango kile tunachokitarajia katika sherehe hizi za Kanda
ya Kati mwaka 2024," amesema Mhe. Senyamule.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego
amesema kikao hiki kitaonesha Dira wapi tumetoka na tunapoelekea na kuna mambo
hayatakiwi kusubiri na kupoteza muda. Kila timu iliyopangwa ihakikishe inafanya
vizuri ili kuondoa sintofahamu hapo mbeleni.
Vile vile, Bi. Aziza Mumba, Katibu Tawala Msaidizi sekta za
Kilimo na Uchumi Mkoa wa Dodoma amesema kila mwaka Agosti Mosi hadi 08,
Serikali hufanya sherehe za Nane Nane kikanda na sherehe za maonesho mahususi
ya wakulima.
"Mikoa ya Singida na Dodoma inayounda Kanda ya Kati,
kupitia sherehe hizi ina lengo la kutangaza fursa za uwekezaji, biashara
sanjari na kusambaza taarifa za teknolojia na mbinu za Kilimo bora zinazoweza
kuwawezesha wakulima kufanya kilimo cha kisasa na kupata mazao stahiki,"
Bi Mumba.
Kikao hicho kimeazimia mambo kadhaa ikiwemo; kamati ndogo ibainishe na kuongeza taasisi za Wizara ya Kilimo na Misitu, Taasisi za Misitu zihusishwe ipasavyo kwani Sekta ya Kilimo inahusisha Mazao, Mifugo, Uvuvi, Madini na Misitu, kuweka Kongamano la siku moja la Uwekezaji litakaloangazia fursa.
0 Maoni