Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi
amewatembelea Mabalozi wa Tanzania wanaoshiriki warsha ya siku 4 ambayo
imekamilika mjini Kibaha jana Aprili 24, 2024 kwa kufikia makubaliano
mbalimbali ambayo yanalenga kuipaisha diplomasia ya Tanzania duniani.
Dkt. Nchimbi aliwapongeza Mabalozi hao kwa kazi nzuri
wanayoifanya ya kuitangaza nchi na kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la
biashara, uwekezaji na utalii nchini.
Warsha hiyo ambayo ililazimika kumalizika usiku kila siku
ilifanyika chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb) ilijadili mikakati ya kuboresha
utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje na namna ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa
changamoto ambazo zimekuwa kikwazo kufikia ufanisi wa shughuli za Wizara hiyo.
Katika siku zao 4, Mabalozi pamoja na mambo mengine,
walipitia mikakati ya Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi, Uendelezaji wa
majengo ya ofisi na makazi ya Balozi, Diplomasia ya Umma na Diplomasia ya
kidigitali na viashiria vya kupima utendaji (Key Performance Indicators- KPIs).
Mabalozi walieleza kuwa kukamilika kwa nyaraka hizo ambazo
hazikuwahi kuwepo Wizarani kabla ni chachu katika mwelekeo mpya wa Utekelezaji
wa Diplomasia ya Uchumi.
Mabalozi walisisitiza umuhimu wa kumaliza changamoto za
kimawasiliano baina yao na wadau ambazo zimekuwa kikwazo za kukamilika kwa
wakati kwa fursa na miradi ambayo imekuwa ikiletwa nchini. Changamoto nyingine
kubwa ambayo Mabalozi wamesisitiza itafutiwe ufumbuzi ni uwezo mdogo wa nchi
yetu wa kuzalisha bidhaa za kukidhi soko katika maeneo yao ya uwakilishi.
Waheshimiwa Mabalozi
walisema kuna soko kubwa la nyama, maparachichi, korosho, mchele na bidhaa
nyingine lakini hakuna bidhaa za kutosha nchini za kulisha soko hilo.
Mabalozi katika warsha hiyo walipata fursa ya kusikiliza
nasaha za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa njia ya mtandao ambaye aliwataka kuwa jicho la Tanzania katika
maeneo yao ya uwakilishi ili nchi isipitwe na mabadiliko yanayotokea duniani.
Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka
alifika katika warsha hiyo na kuwambia Mabalozi kuwa wapo katika Wizara
iliyokusanya watu wenye taaluma, ujuzi, uzoefu na historia ya kutoka sekta
tofauti mchini. Aliwasihi washirikiane kutumia fursa hiyo kuharakisha
mabadiliko ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na kutatua changamoto
zinazowakabili.
Taasisi kadhaa pia zilialikwa na kuwasilisha mada kuhusu
shughuli za ofisi zao ambazo ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mfuko wa
Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Benki ya Azania.
Warsha hiyo pia wakati wa ufunguzi, walikaribishwa Mabalozi
wastaafu ambao walipata fursa ya kubadilishana uzoefu na Mabalozi wa sasa kwa
lengo moja tu la kujengeana uwezo wa kukuza na kuimarisha uhusiano wa
kidiplomasia baina ya Tanzania na mataifa mengine, mashirika ya Kikanda na
Kimataifa.
Waziri Makamba ambaye ana muda wa takribani miezi 7 tokea ahamishiwe Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema Wizara inaweza kufanya zaidi kuliko inavyofanya hivi sasa. Hivyo, warsha hiyo iliandaliwa ili kupigana msasa wa kufikia nchi ya ahadi.
0 Maoni