Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA) Mhandisi Victor Seff ameagiza timu ya wataalamu wa TARURA Makao Makuu
na ya Mkoa wa Pwani kufanya mapitio ya usanifu wa daraja la Bibi Titi
Mohammed-Mohoro linalotarajiwa kujengwa wilayani hapa.
Mhandisi Seff ameyasema hayo mara baada ya kufanya ukaguzi wa
mradi huo na kuona jinsi maji yalivyojaa kutokana na mvua zinazoendelea
kunyesha.
Mhandisi Seff amesema lengo la mapitio hayo ni kuhakikisha
kuwa uwezo wa daraja litakalojengwa litamudu kupitisha maji ya mvua na kutoka
bwawa la Nyerere endapo yatafunguliwa bila kuleta madhara yoyote kwa wananchi.
Aidha,Mhandisi Seff alifanya kikao na viongozi wa Wilaya na
Halmashauri ya Rufiji upande wa pili wa daraja hilo ambao pia walionesha
wasiwasi wao kutokana na historia ya eneo hilo na maji kutoka bwawa la Nyerere
endapo yatafunguliwa wakati mvua zinaendelea kunyesha.
Hata hivyo Mhandisi Seff aliwahakikishia viongozi hao kwamba
mapitio hayo ni kujiridhisha kuwa usanifu uliofanyika unakidhi na kupitisha
maji yatakayoongezeka bila kuleta madhara yoyote.
Daraja la Bibi Titi Mohammed-Mohoro linatarajiwa kuwa la
zege na kukamilika kwake itaenda
kuondoa kilio cha muda mrefu cha wakazi wa vijiji vya Mohoro na Chumbi pamoja
na kuimarisha uchumi.
0 Maoni