Ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango
mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanywa
na Serikali ikiwa ni pamoja na kufanya
Marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Mabadiliko hayo yalifanyika
Mwaka 2017 yalipelekea kuanzishwa kwa Tume ya Madini na kuvunja Wakala wa
Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na TANSORT.
Akielezea uanzishwaji wa Tume ya Madini kwa kifupi Katibu Mtendaji wa Tume, Mhandisi Yahya
Samamba anaeleza kuwa, Tume ya Madini
ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kama ilivyorekebishwa
mwaka 2017 lengo likiwa ni kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Sera na
Sheria ya Madini ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.
Akielezea majukumu ya Tume ya Madini kwa ujumla wake,
Mhandisi Samamba anafafanua ni pamoja na
kutoa na kusimamia leseni za madini, kusimamia shughuli za utafutaji,
uchimbaji, na biashara ya madini, kusimamia ukaguzi wa migodi na mazingira kwa
ujumla.
Mbali na kupongeza juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mhandisi Samamba anaeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa Tume ya
Madini wananchi wengi wameshuhudia mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Madini na
kuongeza imani kwa Rais na Serikali kwa ujumla.
Akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli kabla na baada ya
kuanzishwa kwa Tume, Mhandisi Samamba
anaeleza kuwa ukusanyaji wa maduhuli umeongezeka kutoka shilingi bilioni 213.3
katika kipindi cha mwaka wa fedha
2016/17 hadi shilingi bilioni 677.7 katika kipindi cha mwaka wa fedha
2022/2023.
“Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 kama Tume ya
Madini tulipewa lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 822 na kufanikiwa kukusanya kiasi cha
shilingi bilioni 677.7 ikiwa ni (82.45%)
na katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 tumepewa lengo la kukusanya
kiasi cha shilingi bilioni 882 ambalo ninaamini kabisa tutalivuka,” anasisitiza
Mhandisi Samamba.
Mhandisi Samamba anasema siri ya mafaniko kwenye ukusanyaji
wa maduhuli ni pamoja na uzalendo na ubunifu wa
watumishi wa Tume ya Madini Makao Makuu, Ofisi za Maafisa Madini Wakazi
wa Mikoa, Maafisa Migodi Wakazi na ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa
Wizara ya Madini.
Katika hatua nyingine
akielezea masoko ya madini yaliyoanzishwa nchini, Mhandisi Samamba anasema kuwa
masoko yalianzishwa kama njia mojawapo ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata
soko la uhakika la madini yao baada ya kuchimba, Serikali kupata mapato na
takwimu sahihi za madini yanayozalishwa na wachimbaji wadogo wa madini, kuuza
madini kulingana na bei elekezi inayotolewa na Tume ya Madini kulingana na soko
la dunia. Vilevile kudhibiti utoroshaji wa madini kwa wachimbaji na wafanyabiashara
wasio waaminifu.
Anaendelea kusema kuwa mpaka sasa Tume ya Madini ina masoko
ya madini 42 na vituo vya ununuzi wa madini 99 nchini ambayo yameongeza mchango
wa wachimbaji wadogo wa madini kwenye mapato kutoka asilimia tano (5) hadi
asilimia arobaini (40) Mwaka 2022/2023.
Anasisitiza kuwa masoko ya madini yamepunguza kwa kiasi
kikubwa kasi ya utoroshaji wa madini pamoja na kuleta ushindani kwa
wafanyabiashara wa madini kupitia masoko na vituo vya ununuzi wa madini.
Akielezea mikakati ya Serikali katika udhibiti wa utoroshaji
wa madini na kuhakikisha thamani ya madini ya tanzanite inazidi kuimarika,
Mhandisi Samamba anasema kuwa mnamo mwaka 2018 Serikali iliamua kujenga ukuta
wa Mirerani uliopo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara ambao umekuwa na manufaa
makubwa kwa wachimbaji wa madini hayo na Serikali kwa ujumla.
Anaeleza kuwa mikakati mingine iliyowekwa na Serikali ni
pamoja na kuwahamisha wafanyabiashara wa madini kutoka jijini Arusha hadi
Mirerani lengo likiwa ni kuinua uchumi wa eneo la Mirerani na kudhibiti
utoroshaji wa madini.
Aidha, anasimulia kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini
inaandaa mfumo maalum wa kudhibiti mnyororo mzima wa madini ya tanzanite
kuanzia kwenye uchimbaji, biashara, uongezaji thamani hadi usafirishaji wake
lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa thamani ya madini hayo inazidi kupaa duniani.
Katika hatua nyingine akielezea namna serikali inavyosimamia
suala la ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini anasema kuwa kwa
kutambua umuhimu wake, mwaka 2018 serikali iliweka kanuni na miongozo
mbalimbali ya kuhakikisha watanzania wanashiriki katika shughuli za utafiti na
uchimbaji wa madini kupitia utoaji wa huduma mbalimbali kwenye migodi ya madini
kama vile usafiri, bidhaa za kilimo, ulinzi, bima, sheria, benki, n.k.
Anasema mpaka kufikia
mwaka 2022 asilimia 86 ya bidhaa na huduma zinatolewa na kampuni za kitanzania
kwenye kampuni kubwa za uchimbaji wa madini huku asilimia 14 zikitolewa na
kampuni za nje ya nchi kupitia kibali maalum kinachotolewa na Tume ya Madini na
kwa upande wa ajira katika migodi ya madini asilimia 96 ni watanzania huku raia
wa kigeni wakiwa ni asilimia (4) nne.
“Ieleweke kuwa hakuna kampuni yoyote inayoruhusiwa kuagiza
bidhaa au huduma kutoka nje ya nchi bila kupata kibali kutoka Tume ya Madini,
lengo letu ni kuhakikisha kila mtanzania ananufaika na Sekta ya Madini,”
anasisitiza Mhandisi Samamba.
Katika hatua nyingine Tume ya Madini imekuwa ikisimamia kwa
makini katika kuhakikisha kampuni za
uchimbaji wa madini zinatoa huduma kwa jamii (CSR) inayozunguka machimbo
yake kama Sheria ya Madini inavyoelekeza.
Mhandisi Samamba anadokeza kuwa katika mafanikio kwenye Sekta
ya Madini suala la usalama kwenye migodi
haliwezi kuachwa nyuma, na katika kutambua hilo Tume ya Madini kupitia
Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira imekuwa ikifanya kaguzi za mara kwa
mara kwenye migodi ya madini pamoja na kutoa elimu.
Anaendelea kutaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na ongezeko la utoaji wa leseni za madini kutoka
leseni 5094 katika mwaka wa fedha 2018/2019 hadi leseni 9642 katika mwaka wa
fedha 2022/2023.
Anaongeza kuwa mchango wa Sekta ya Madini kweye Pato la Taifa
uliongezeka kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017 hadi asilimia 9.1 mwaka 2022.
Mhandisi Samamba anahitimisha kwa kusema kuwa kampuni nyingi
za kigeni zimeendelea kuonesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya Madini kutokana
na kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Samia Suluhu Hassan ya kutangaza fursa zilizopo nchini.
0 Maoni