Katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, bajeti ya kuboresha miundombinu
chini ya TARURA takribani Trilioni 2.53 zimepokelewa kwaajili ya uboreshaji wa
miundombinu ya barabara za vijijini na mijini.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI,
Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akielezea mafanikio ya miaka mitatu ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mkoani Dar es Salaam.
Mhe. Mchengerwa alisema nyakati ambayo Serikali imefanya kazi
kubwa upande wa miundombinu ni kipindi cha Awamu ya Sita ndio maana Rais
aliliona hilo na kuongeza bajeti ya TARURA.
Alitaja mafanikio ya ujenzi wa barabara za lami na miradi ya
kimkakati, zimejengwa barabara za Lami Km 819.22 ambazo zimeongeza mtandao wa
barabara za lami toka Km 2,404.90 hadi Km 3,224.12.
“Wakati wa Baba wa Taifa alipoanzisha msingi wa kukuza miji
kupitia dhana ya ujamaa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu
Hassan imeendeleza misingi ya Hayati
Mwalimu Julius Nyerere.”
Kwa upande wa ujenzi wa barabara za changarawe Waziri
Mchengerwa alisema Km 11,924.36 zimejengwa na kuongezeka mtandao wa barabara za
changarawe toka Km 29,183.17 hadi Km 41,107.52 na ujenzi wa Madaraja Wakala
imejenga madaraja makubwa sita (6) ambayo ni ya Berega (140m) -(Kilosa,) Msadya
(60m) -(Mpimbwe DC), Mwasanga (40m)- (Mbeya) yamejengwa na yanatumika.
“Rais amewagusa wananchi wengi wa vijijini kwa ujenzi wa madaraja ya Kiwila-(40m)-Ileje, Mkomanzi-Korogwe
(60m) na Kalambo (80m)-(Kalambo) ujenzi ambao unaendelea kukamilishwa,
tunawapongeza TARURA.”
Aidha, alitaja mafanikio mengine ni ujenzi wa barabara na
madaraja kwa kutumia malighafi za ujenzi zinazopatikana maeneo ya kazi
zinapotekelezwa kama mawe, matofali ya kuchoma, ujenzi wa barabara kwa kutumia
mawe.
“Mpaka sasa jumla ya Km 23.18 za Barabara ya Mawe zimejengwa
kwa gharama ya bilioni 8.1 ambapo ni sawa na bilioni 12.8 kama tungetumia lami
nyepesi (double surface dressing) na bilioni 33.6 kama tungetumia lami ya zege
(Asphat Concrete),” aliongeza kusema.
Vilevile, alisema
ujenzi wa madaraja kwa kutumia mawe ni mojawapo ya kipaumbele cha TARURA ni
kutumia malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi ili kupata ufanisi wa gharama
za ujenzi.
Hata hivyo, alisema hadi Mwezi Februari, 2024 TARURA imejenga
madaraja 226 ya mawe yenye thamani ya bilioni 12.52 ambapo gharama imepungua
kwa zaidi ya asilimia 50.
Wakala unaendelea kufanya majaribio ya teknolojia mbalimbali
ili kutumia udongo uliopo eneo la kazi badala ya kusomba kutoka maeneo mengine
ya mbali.
Hadi sasa kwa kutumia Teknolojia ya ECOROADS zimejengwa Km 22
na ujenzi upo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.
Naye, Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary
Kumbilamoto alisema ndani ya miaka mitatu mradi wa DMDP kwa wilaya ya Ilala
umeweza kuondosha kero za barabara kwa wakazi wengi wa Ulongoni hadi
Gogolamboto ambao awali walijiona wametengwa.
Alisema walipata bilioni 17.6 kwa ajili ya ujenzi wa barabara
na mifereji na hivyo kuweza kuondoa changamoto na kuifanya Ilala kufunguka.
Wakati huo huo Naibu Meya wa Kinondoni, Mhe. Joseph Rugasira
alisema DMDP-1 walipata ujenzi wa barabara Km 55 na mitaro zaidi ya Km 8.9 na
kufanya maeneo mengi ya Mwananyamala, Tandale na Kinondoni kwa ujumla kupendeza.
“Tunampongeza Mhe. Rais kwani DMDP-2 itaenda kutatua
changamoto za barabara na wananchi wanafurahia kuona maendeleo katika
miundombinu.”
Na. Catherine Sungura- Dar es Salaam
0 Maoni