Mamlaka ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania
(TAWA), imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 184.74 katika kipindi
cha kati ya mwaka 2020/21 hadi 2024.
Hayo yamesemwa na Kamisha wa Uhifadhi na Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA), Kamishna Mabula Misungwi Nyanda, Jijini Dar Es
Salaam Machi 18, 2024, wakati akitoa wasilisho la mafanikio ya TAWA kwa kipindi
cha miaka mitatu (2021/22-2023/24 ) ya serikali ya awamu ya sita ya uongozi wa
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema juhudi za makusudi zilizofanywa na Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, kutangaza utalii kupitia filamu ya Royal Tour, Fedha za UVIKO 19
chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19
(Tanzania Social Economic Response and Recovery Plan (TCRP ) ambapo TAWA
imefaidika kwa kuimarisha miundombinu wezeshi ya Utalii katika maeneo
mbalimbali.
Ametaja maeneo hayo ni pamoja na ujenzi wa Kilomita 431.4 za
barabara katika Mapori ya Wamimbiki, Mpanga Kipengere, Igombe, Swagaswaga,
Mkungunero, Kijereshi, Rungwa na Pande,
Aidha, TAWA pia imeweza kukarabati viwanja vya ndege vitatu
(3) katika Pori Tengefu Lake Natron (Engaresero) na Pori la Akiba Maswa (Buturi
na Mbono),
Pia, kujenga miundombinu ya kupumzika wageni (Bandas 13,
Campsites - 6, picnic sites - 8, lounge 1) na hostel 1 katika Mapori ya Akiba
Mpanga Kipengere, Mkungunero, Lukwika Lumesule, Pande Swagaswaga na Magofu ya
Kilwa.
Kamishna Nyanda pia amesema, mafanikio mengine ni pamoja na
ujenzi wa malango matano (5) na vituo vinne (4) vya kukusanyia mapato katika
Mapori ya Akiba ya Wamimbiki, Mkungunero, Lukwika Lumesule, Swagaswaga, Mpanga
Kipengere, Kijereshi na katika Pori Tengefu Ziwa Natron,
Ujenzi wa njia ya waenda kwa miguu zenye urefu wa kilometa
3.7 katika Pori Tengefu Ziwa Natron, na Mapori ya Akiba Swagaswaga, Kilwa
Kisiwani na Mpanga Kipengere,
Miundombinu mingine iliyoimariswa ni ukarabati wa mabanda
sita (6) ya Utalii katika Pori la Akiba Wamimbiki.
Aidha, Kamishna Nyanda amesema kumekuwepo na ongezeko la
Wawindaji kutoka 355 mwaka 2020/21 hadi wawindaji 787 mwaka 2022/23 na
wawindaji 481 hadi Februari mwaka 2024, lakini pia kuongezeka kwa idadi za meli
za Kimataifa za utalii kutembelea eneo la Kihistoria Kilwa.
0 Maoni