Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amesihi
wawekezaji kutoka Mataifa mbalimbali (USA) kuwekeza katika sekta ya nishati
nchini ikiwemo eneo la nishati safi ya kupikia, nishati jadidifu pamoja na gesi
ili kuendelea kuchochea maendeleo katika nyanja tofauti tofauti.
Kauli hiyo imetolewa jana katika Ofisi Ndogo ya
Wizara iliyopo jijini Dar es Salaam alipofanya kikao na Naibu Waziri mdogo wa
Nishati wa Marekani, Mhe. Joshua Volz kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu ambaye pia
ni Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko.
Mhe. Kapinga amesema kuwa Tanzania ni sehemu salama ya
kuwekeza hususan katika Sekta ya Nishati ambapo ameeleza kuwa Tanzania ipo
tayari kupokea wawekezaji katika sekta ya nishati ili kuongeza tija kwenye
maendeleo ya Nchi.
‘’Tanzania ina vyanzo
vingi vya umeme ikiwemo nishati jadidifu kama vile Upepo, Jua na Jotoardhi,
ndio maana nachukua nafasi hii kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchi ya Marekani
wajitokeze kuwekeza katika sekta ya nishati hapa nchini,” amesema Mhe. Kapinga.
Amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya
umeme inayotokana na Nishati Jadidifu kama vile Mradi wa umeme Jua Shinyanga
ambao unatarajia kuzalisha megawati 150 baada ya kukamilika, Mradi wa kuzalisha
umeme kwa kutumia Upepo uliopo Singida na Miradi ya Jotoardhi iliyopo katika
Mikoa ya Songwe na Mbeya.
Mhe. Kapinga amesema Tanzania inaendelea na hatua za utekekelezaji
wa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao unategemea
kuzalisha jumla ya megawati 2,115 na utekelezaji wake umefikia asilimia 96.
Pia, viongozi hao wamejadiliana kuhusu utekeleza miradi ya
kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme inayotekelezwa nchini ili kuhakikisha
umeme unafika maeneo mbalimbali nchini na kuvutia wawekezaji katika nyanja
tofauti tofauti, pia wemezungumzia miradi kusafirisha umeme kati ya Tanzania na
nchi nyingine.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati wa Marekani, Mhe.
Joshua Volz ameonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika kuwekeza kwenye
sekta ya nishati nchini ikiwemo miradi ya umeme na gesi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Watendaji kutoka Wizara ya
Nishati, Wizara ya Mambo ya Nje, viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati
ya Marekani na viongozi waandamizi wa Ofisi ya Ubalozi wa Marekani nchini
Tanzania.
0 Maoni