Ajali ya barabarani yaua wawili na kujeruhi Askari wa Zimamoto

 

Watu wawili wamepoteza maisha na wengine watano kujeruhiwa nkatika ajali iliyohusisha magari matatu likiweno basi la abiria la kampuni la New Force na Sauli pamoja na lori la mafuta na kuteketea kwa moto leoa alfajiri Machi 28 eneo la Mlandizi, mkoani Pwani.

Miongoni mwa watu watano waliojeruhiwa ni pamoja na askari wawili wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambao wamejeruhiwa wakati wakiwa watatekeleza majukumu yao ya uokoaji.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Pius Lutumo ameeleza kuwa gari namba T 668 DTF aina ya scania kampuni ya Sauli ikiendeshwa na Iddi Aloyce (35) mkazi wa Mafinga likitokea Dar kuelekea Mbeya liligonga ubavuni lori la mafuta ya petrol lenye namba za usajili RAF672N na tela lenye namba RL2594 aina ya Howo lililokuwa linatoka Dar es Salaam kwenda Rwanda likiendeshwa a Mushimana Musiyimana lililokuwa limesimama kupisha gari lililokuwa linakuja mbele yake.

Amesema basi hilo lilikuwa limeongozana na basi la Golden Deer la kampuni ya New Force lenye namba za usajili T175 DZU likiendeshwa na Burton Jacob (33) mkazi wa Mbeya ambapo nalo liligonga kwa nyuma basi la Saul lililokuwa mbele na kusababisha vifo.

Kamanda Lutumo amesema watu waliofariki bado hawajafahamika majina yao na waliojeruhiwa watatu ni Salim Daud (50) mkazi wa Mbozi, Farida Idrisa (26) mkazi wa Tabata na Kiambile Geoffrey mkazi wa Uyole Mbeya.

“Baada ya ajali hiyo Jeshi la Polisi wakiwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakiwa katika harakati za kuwatoa marehemu waliokuwa wamenasia kwenye gari ghafla magari yaliwaka moto uliotokana na petroli iliyokuwa inavuja toka kwenye tenki la mafuta,” amesema Kamanda Lutumo.

Ameeleza kuwa mlipuko huo ulisababisha majeraha kwa askari wawili wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambao ni Koplo Hamis Kungwi na Koplo Elias Bwire ambao walikimbizwa hospital ya Mloganzila kwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.

Kamanda Lutumo ameeleza kuwa chanzo cha ajali ni uzembe wa madereva wa mabasi yote mawili kushindwa kuchukua tahadhari kwa kuyapita magari mengine lakini pia kushindwa kutunza umbali kati ya gari moja na lingine yakiwa yanafuatana.

Amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya injini ya basi la Sauli iliyokuwa imekita chini baada ya kugonga gari lingine na kulipuka moto wa petroli wakati wa uokoaji.

Chapisha Maoni

0 Maoni