Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali
pamoja na wadau inaandaa mfumo wa rufaa kwa wahamaji walio katika mazingira
hatarishi nchini utakaosaidia kutoa huduma kwa makundi maalum wakiwemo watoto.
Hayo yamebainika wakati wa kikao kilichowakutanisha
Wakurugenzi na Makamishna kutoka Wizara za Kisekta na wadau mbalimbali kujadili
uandaaji wa mfumo wa rufaa kwa wahamaji walio katika mazingira hatari Machi 27,
2024 jijini Dodoma.
Akifungua kikao hicho Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Nandera
Mhando amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua mchango
unaotolewa na wadau katika kuhudumia makundi yenye uhitaji wakiwemo wahamaji
walio katika mazingira hatarishi hivyo kama Wizara yenye dhamana na makundi
maalum wakiwemo watoto imeona ni vema kuwa na mfumo wa rufaa kwa wahamaji walio
katika mazingira hatarishi hususan watoto ili kuhakikisha kuwa kundi hili nalo
linapata huduma stahiki kwa wakati.
Ameongeza, kuwepo kwa mfumo huo kutasaidia ushirikiano kati
ya Wizara za Kisekta,Taasisi za Serikali na wadau katika kutoa huduma kwa
wahamaji walio katika mazingira hatarishi ambapo huduma hizo zinajumuisha
kuwaunganisha na nchi zao watoto
waliovuka mipaka na kuingia Tanzania ikiwa ni pamoja na wale walio katika
mkinzano na Sheria kwa kosa la kuingia nchini kinyume na Sheria.
"Kikao hiki ni cha muhimu sana kwetu na niombe tukipe
uzito mkubwa kwani tutakayo yajadili leo yatatuwezesha kuimarisha ushirikiano
kati ya taasisi zetu za Serikali na wadau katika kuwapatia huduma wahamaji
ambao ni walengwa wa mfumo huu ambapo baadhi yao ni watoto waliokinzana na
Sheria kwa kuingia nchini kinyume cha Sheria, watoto waliotengana na wazazi wao
na wale waliovuka mipaka bila ya kuwa na uangalizi," amesema Dkt. Nandera.
Kamishna Dkt. Nandera amesisitiza kwamba kuna umuhimu wa kuwa
na mfumo wenye uratibu mzuri utakaosaidia wadau wote kutimiza wajibu wao kwa
wakati pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa walengwa. Hivyo amewaomba
wadau kutoa michango na maoni ya kitalam yatakayowezesha kuwa na mfumo mzuri wa
rufaa utakaosaidia upatikanaji wa huduma kwa wahamaji walio katika mazingira
hatarishi hapa nchini.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri
Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Honesta Ngolly ameshauri kamati ya
uandaaji mfumo huo kuhakikisha wanatoa elimu kwa watumiaji na wadau wengine ili
kuwa na mfumo utakaojumuisha walengwa wote ili kuondokana na changamoto katika
kupata rufaa kwa wahamaji walio katika mazingira hatarishi nchini.
Naye Afisa Programu Msaidizi kutoka Shirika la IOM Ken Heriel
amesema Shirika hilo limeamua kushirikiana na Serikali kuwa na mfumo
utakaosaidia kuwa na namna bora ya utoaji huduma za rufaa kwa wahamaji
waliokatika mazingira hatari ili kuwasadia kupata huduma muhimu wakati wakiwa
katika njia ya uhamiaji.
Na. WMJJWM- Dodoma
0 Maoni