Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
imeipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa utekelezaji wa
mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) katika halmashauri ya Mji
wa Nzega mkoa wa Tabora.
Kauli hiyo imetolewa jana 27 Machi 2027 wilayani Nzega na Makamu
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe, Japhet Hasunga wakati wa ziara ya Kamati yake
kukagua hatua iliyofikiwa katika Utekelezaji mradi wa LTIP kwenye halmashauri
ya Mji wa Nzega mkoani Tabora.
Mradi wa LTIP katika Halmashauri ya Mji wa Nzega umepewa
lengo la kurasimisha vipande vya ardhi 20,000 na kuongeza alama za msingi za
upimaji 14.
"Niwapongeze kwa kazi hii mlioamua kuifanya tangu tupate
uhuru tumekuwa na changamoto za ardhi kuanzia kutambua, kupima, kurasimisha na
kadhalika, kumekuwa na shida," amesema Mhe, Hasunga.
Amesema, Mhe, Rais ameamua kutoa fedha nyingi za mradi wa
LTIP na Bunge kuidhinisha ambapo kwa upande wa halmashauri ya Mji Nzega kiasi
cha Shilingi Bilioni 1.4 kimeidhinishwa kwa ajili ya Kata tano hivyo wananchi
watumie fursa ya kutambuliwa maeneo yao na hatimaye kupatiwa hati kupitia mradi
huo.
Ameeleza kuwa, Kamati yake ya PAC itakwenda kupima thamani ya
fedha zilizopitishwa na Bunge pale tu wananchi watakapokuwa na hati.
"Msipopata hati hii mingine yote ni michakato, sisi
hatuhitaji michakato tunataka kuona watu wangapi wana hati," alisema Mhe,
Hasunga.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe,
Geophrey Pinda amesema, wizara yake ina uhakika michakato yote itakapokamilika
katika mji wa Nzega hati milki za ardhi zitaenda kutolewa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Mhe, Pinda utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji
Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaenda kutoa jumla ya hati milki za ardhi
1,500,000 kwa maeneo yote yanayopotiwa na mradi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga ameweka wazi kuwa, kazi iliyofanyika
kwa halmashauri ya Mji wa Nzega kwa sasa imefikia asilimia 55 na kiasi cha
fedha kilichotolewa ni asilimia 39.
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP)
unatekelezwa kwa mkopo wenye thamani ya Dola za Kimarekani milionin150 kutoka
Benki ya Dunia kwa kupindi cha miaka 5 katika halmashauri 58 nchini. Mradi huo
unalenga kuboresha utawala na usimamizi wa ardhi nchini pamoja na kuongeza
usalama wa milki za ardhi kwa wananchi.
Na. Munir Shemweta- Nzega
0 Maoni