WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania
imeshuhudia magaeuzi na maboresho makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa
katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Sukuhu Hassan.
Amesema kuwa matokeo ya jitihada hizo ambayo kwa kiasi
kikubwa yameimarisha ustawi wa Watanzania yanapaswa kuungwa mkono na kila
mtanzania bila kujali itikadi ya vyama vyetu. “Kazi yake kubwa tumeiona,
matunda ya kazi yake yamekuwa na manufaa kwetu sote.”
Amesema hayo jana kwenye Kongamano la Kurasa 365 za Samia
lililoratibiwa na Kampuni ya Clouds Media kwenye ukumbi wa mikutano wa Mlimani
City jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo lililenga kuonesha mafanikio ya miaka
mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Madarakani.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia katika
kipindi cha miaka mitatu ameendeleza miradi yote ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa
Reli ya Kisasa (SGR), ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere ambalo
limeanza kuzalisha umeme na kuingiza katika gridi ya Taifa, uendelezaji wa mji
wa Serikali.
Miradi Mingine ni Ujenzi wa Madaraja Makubwa ya Mfano ikiwemo
Kigongo-Busisi ambao ujenzi wake umefikia asilimia 85 na Ujenzi wa Meli ya MV.
Mwanza “Hapa Kazi Tu” ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 93 na imeshaanza
majaribio.
Amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameendelea kuwa kinara katika
kuendeleza diplomasia ya uchumi ambayo kwa yameiwezesha Tanzania kupanua wigo
wa uwekezaji “Kitendo hiki cha Rais Dkt. Samia kuhamasisha mataifa ya nje
kujenga urafiki wa karibu na Tanzania yametuwezesha kufanikiwa kwenye maeneo ya
utalii uwekezaji, mitaji, masoko ya bidhaa, ongezeko la watalii, na utatuzi wa
changamoto za kibiashara na nchi jirani.”
Akizungumzia Sekta ya Elimu Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa
kwa sasa Serikali inakamilisha ujenzi wa shule za msingi katika kila kijiji kwa
lengo la kumuwezesha mtoto wa Kitanzania atembee umbali mfupi kufuata shule
“Sekondari tulianza na mpango wa kata na tunaendelea kuongeza shule.”
Aidha, Amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameendelea kufungua
milango kwa sekta binafsi kushiriki katika masuala ya maendeleo nchini
“Ninataka miwahakikishie watanzania, tunaendelea kufungua mipango kwa sekta
binafsi na kutengeneza sera rafiki kwa ustawi wa Taifa letu.”
Amesema kuwa Serikali imeimarisha huduma za afya kuanzia
vijijini kwenye zahanati mpaka hospitali za kitaifa pamoja na ujenzi wa
hospitali za kanda kwa kupeleka dawa, vifaa tiba na vitendanishi “Tumejenga
hospitali za kanda ambazo kwa sasa zinatoa huduma hata kwa wagonjwa kutoka nchi
jirani.”
Amesema katika Sekta ya Maji Rais Dkt. Samia amewekeza fedha
kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji akiwa na lengo la
kuhakikisha kila mtanzania ananufaika na uwepo wa huduma ya maji safi na salama
“Rais Dkt. Samia ametoa fedha kwa ajili ya kununua mitambo ya kugundua maeneo
yenye maji, pamoja na mitambo ya kuchimba visima, lengo lake ni kupeleka maji
kwenye kila kijiji.”
Aliongeza
kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatambua umuhimu wa sekta ya kilimo katika
kukuza uchumi wa nchi yetu “Moja kati ya jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais Dkt
Samia amelifanya ni kuongeza bajeti kwenye sekta ya kilimo ili iweze kusimamia
kikamilifu sekta hii.”
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Stephen Kiruswa amesema kuwa
Sekta ya Madini ni muhimu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa na kuwqletea
watanzania mmoja mmoja mafanikio katika kukuza uchumi wao “Kimsingi utajiri
tulionao wa madini ni mkubwa sana na tutaendelea kusimamia sekta hii kikamilifu.”
Naye, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa katika kipindi
cha miaka mitatu Rais Dkt. Samia amewekeza katika sekta ya afya kwa ununuzi wa
vifaa vya kisasa, na ujenzi wa miundombinu ya afya ambayo kwa kiasi kikubwa
imesaidia kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni