Idadi ya watalii imeendelea kuongeza hapa nchini, ikiwa ni
matokeo ya filamu ya Royal Tour, ambayo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuwa mshiriki mkuu.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa
Serikali, Bw. Mobhare Matinyi amesema hayo jana Machi 10, 2023 jijini Dodoma
wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu maendeleo ya utalii na
miundombinu baada ya mvua za El Nino katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Idadi ya watalii wanaokuja nchini imekwenda juu kupita
malengo makubwa yaliyowekwa kwa mwaka huu wa fedha. Taarifa ya mafanikio hayo
ni kwamba, ingawa makadirio ya idadi ya watalii kwa hifadhi zote za TANAPA kwa
mwaka 2023/24 yalikuwa 1,387,987 lakini mpaka kufikia Februari 2024 (miezi nane
tu kuanzia Julai 2023), jumla ya watalii 1,451,383 wameshaingia huku Serengeti
ikiwa na watalii wengi zaidi,” amesema Bw. Matinyi.
Watalii hao wametoka maeneo mbalimbali ya dunia, ambapo
watalii kutoka nje ya nchi za Afrika Mashariki ni 749,365, watalii wageni
lakini wakaazi wa nchini Tanzania ni 10,531, watalii wa Afrika Mashariki
230,785 ambapo kati ya hao watalii 127,650 ni Watanzania, pamoja na wafanyakazi
wa hoteli, kambi na madereva 460,702.
Kwa upande wa miundombinu amesema kuwa, hifadhi za taifa 21
zilizo chini ya TANAPA zina barabara zenye urefu wa jumla ya kilomita 16,470.6
ambapo Serengeti peke yake ina jumla ya kilomita 3,176, ikiwa ni hifadhi yenye mtandao mrefu zaidi wa
barabara ambazo ni za udongo ama changarawe.
“Barabara hizi zimegawanyika katika barabara kuu zilizo chini
ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na
Mijini Tanzania (TARURA) na kundi la pili la barabara ndogondogo zilizo chini
ya TANAPA yenyewe. Serengeti pia ina viwanja vidogo vya ndege (airstrips)
vipatavyo saba ambavyo ni Serengeti, Kogatende, Lobo, Lamai, Grumeti, Kusini na
Fort Ikoma,” amesema Bw. Mobhare.
Aidha, amesema kuwa TANAPA huzitunza barabara hizo na viwanja
vya ndege ili kuhakikisha watalii wanaendelea kuingia hifadhini, ambapo hutumia
wataalam wake pamoja na vifaa vyake. Kwa mujibu wa sera yake ya uhifadhi,
TANAPA hutumia changarawe kutoka ndani ya hifadhi kwa ajili ya matumizi
endelevu, kupunguza gharama na kuepuka kuingiza mimea-vamizi ambayo huharibu
malisho ya wanyama na pia kuleta magonjwa ya mimea.
“Pale ilipotokea changamoto ya mvua za El Nino kulitokea
mafuriko makubwa hifadhini kiasi cha kufunika barabara kuu zinazoleta watalii.
Uharibu ulikuwa mkubwa. Hivyo basi, TANAPA ilichukua hatua za haraka za awali
za kuzifanyia matengenezo barabara hizo ili kuhakikisha kwamba wageni
wanaendelea kutalii na usafirishaji haukwami,” amesema Bw. Matinyi.
Ameendelea kusema kuwa, TANAPA katika hatua za awali
imekamilisha matengenezo na sasa barabara hizo zinapitika na watalii
wanaendelea kupata huduma zinazostahili. Amesema, “Hakuna changamoto kubwa
iliyotokea kwenye upande wa viwanja vidogo vya ndege saba vilivyopo zaidi ya
maji kujaa kwenye baadhi ya maeneo ya kuegeshea ndege. Hivyo baada ya maji hayo
kukauka, huduma ziliendelea kwa usalama”.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeshinda Tuzo ya Hifadhi Bora
Afrika kwa miaka mitano mfululizo. Serengeti ni maarufu zaidi kwa tukio la
uhamaji wa wanyama aina ya nyumbu ambapo kila mwaka nyumbu wapatao milioni 1.5 hutumia
miezi kumi wakizunguka ndani ya hifadhi ya Serengeti na kisha kwenda nchi
jirani na kurejea. Katika uhamaji huo tukio la kusisimua zaidi ambalo ndilo
huvuta watalii wengi ni lile la kuvuka mto Mara pamoja na matawi yake.
Na. Lilian Lundo- Idara ya Habari (Maelezo)
0 Maoni