NHC yatoa vyakula vya futari kwa kituo cha Al Madina

 

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limetoa msaada wa vyakula mbalimbali kwa Kituo cha Mafunzo ya Watoto Al Madina kilichopo Msakuzi, Mbezi Mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya futari kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwenye kipindi hiki wakiwa katika funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mbezi Mkoani Dar es Salaam Afisa Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa, Yamlihery Ndullah amesema jukumu la kutoa msaada kwa watoto hao ni jukumu la jamii nzima kwani katika watoto hao watapatikana viongozi wa dini na Taifa hapo baadaye.

Aidha, Ndullah amesema jambo hilo ni muendelezo wa Shirika katika kuendelea kutoa misaada kwenye sehemu mbalimbali zenye mahitaji, pia kupitia kwa Mkurugenzi wa NHC Hamad Abdalah, wataendelea kutoa misaada hiyo ili kuendelea kupeleka faraja na furaha kwa watu wote Nchini.

Kwa upande wake, Imamu wa Msikiti wa Al Madina Sheikh Jumaa Salum Mhando ambaye kituo hicho kipo chini yake  amelishukuru Shirika la Nyumba la Taifa kwa msaada huo mkubwa ambao utawasaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu kuweza kufuturu na kufunga funga zao vyema katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.

"Lengo ni kuwawezesha na kuwakamua katika hali ya kimaisha kwa kuwa wanaishi kwenye mazingira magumu, hivyo tunawapongeza NHC kwa kuleta neema hii katika mwezi maalumu kwa sababu mwezi huu ni mwezi wa kuchuma heri nyingi, waliofanya hivi Mungu atawazidishia zaidi ya hapa na Mungu atawajalia wepesi katika shughuli zao," amesema Sungura.

Hivyo, Imamu wa Msikiti wa Al Madina Sheikh Jumaa Salum Mhando ametumia nafasi hiyo kuwaomba wadau mbalimbali kuwasaidia katika kutoa sadaka ambazo zitawasaidia kuwakwamua watoto ambao wanapitia wakati mgumu, pia kuwasaidia katika kumalizia jengo hilo la msikiti ambalo bado halijakamilika.

Chapisha Maoni

0 Maoni