Mwishoni mwa juma lililopita, Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH) ilimfanyia upasuaji kwa njia ya matundu madogo (Laparoscopic Hellers
Myotomy) mtoto wa miaka saba ambaye alikua na tatizo la kumeza linalojulikana
kwa kitaalam kama Achalasia Cardia tangu akiwa na umri wa mwaka moja kutokana
na mishipa yake ya fahamu ya koo la chakula kuharibika na kumfanya ashindwe
kumeza kwa urahisi.
Daktari Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Mfumo wa Chakula, Ini na
Mbobezi wa Upasuaji wa Matundu Madogo Dkt. Kitembo Kibwana ambaye ameongoza
jopo la watalaam wenzake amesema upasuaji huo ulifanyika ili kupunguza kizuizi
kati ya umio (koo la chakula) na tumbo na kugawanya safu ya misuli kutoka
kwenye umio hadi tumbo ili kumuwezesha mtoto huyo kumeza chakula kwa urahisi.
Dkt. Kibwana amesema Achalasia ni ugonjwa ambao hufanya iwe
vigumu kwa chakula na kioevu kupita kutoka koo la kumeza linalounganisha kinywa
na tumbo (umio) ndani ya tumbo na kuongeza kuwa tatizo hili hutokana na mishipa
kwenye umio kuharibiwa na mwili wenyewe (auto-immune) au baadhi ya maambukizi
na kusabaisha umio kupooza na kupanuka kwa muda na hatimaye kupoteza uwezo wa
kukamua chakula hadi tumboni na matokeo yake chakula hicho hujikusanya kwenye
umio, wakati mwingine huchacha na kurudishwa hadi mdomoni kikiwa na ladha
chungu.
Amewataka wananchi wenye changamoto ya kumeza (Achalasia)
kufika Hospitali ili kufanyiwa uchunguzi na kisha kupatiwa matibabu stahiki
kwani huduma hiyo hutolewa kwa muda mfupi na kumruhusu mgonjwa ndani ya siku
angalau mbili kwenda nyumbani kuendelea na shughuli zake.
“Mpaka sasa tumeweza kufanya upasuaji wa aina hii kupitia
njia ya matundu (Laparoscopy) kwa wagonjwa wapatao 24 kwa ufanisi mkubwa zaidi
ambapo kati ya hai, 3 ni watoto,” ameeleza Dkt. Kibwana.
0 Maoni