Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi ameeleza hadi sasa
maandalizi ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru yamefikia zaidi ya asilimia
90 huku akihimiza Mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha unahamasisha wananchi
kushiriki kwa wingi katika tukio hilo la kihistoria.
Amesema hayo wakati akikagua maandalizi ya uzinduzi wa Mbio
za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa michezo wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi
(MoCU), Mkoani Kilimanjaro.
Aidha, Naibu Waziri Katambi amesema kuwa Mbio hizo za Mwenge
wa Uhuru kwa mwaka huu 2024 zinaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa rasmi mwaka
1964 zikienda sanjari na Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na
Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Vile vile, Mhe. Katambi ameupongeza mkoa huo kwa utayari na
maandalizi mazuri ya tukio hilo la kitaifa na kuongeza kuwa mwenge huo ni alama
ya umoja, hivyo utakimbizwa katika halmashuri 195 kwa lengo la kuunganisha
wananchi sambamba na kukagua viwango vya utekelezaji wa miradi ya serikali
katika kuwahudumia wananchi.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo Zanzibar, Fatma Rajab amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na
Wizara hiyo wamekua wakishirikiana kwa karibu na ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo wa
Kilimanjaro katika kuhakikisha maandalizi yanakamilika ndani ya muda
uliopangwa.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro,
Mhandisi Jackson Masaka amesema kuwa viongozi wa mkoa wamekua na utaratibu wa
kukutana na makundi mbalimbali ya wananchi ikiwemo Bodaboda, Wazee,
Wafanyabiashara, Wanawake kwa lengo la kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi
katika uzinduzi huo.
Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka 2024 zinaogozwa na
kauli mbiu isemayo “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”.
Na. Mwandishi Wetu- Kilimanjaro
0 Maoni