Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amekutana na
kuzungumza na ujumbe kutoka Marekani uliongozwa na Naibu Waziri wa Nishati wa
Nchi hiyo Joshua Volz ambapo pia ameambatana na viongozi waandamizi kutoka
Wizara ya Nishati ya Marekani pamoja na viongozi waandamizi wa Ofisi ya Ubalozi
wa Marekani nchini Tanzania.
Kikao hicho, kimefanyika leo Machi 27, 2024 katika Ofisi
Ndogo Wizara hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Akizunguza katika kikao hicho, Dkt. Kiruswa amesema Tanzania
ni sehemu sahihi na salama ya Uwekezaji hususan katika Sekta ya Madini ambapo
ameueleza ujumbe huo kuwa Serikali ya Tanzania iko tayari kulinda wawekezaji
ili kuongeza tija katika maendeleo ya taifa.
Aidha, Dkt. Kiruswa amesema mpaka sasa nchi ya Tanzania
imefanyiwa utafiti wa kina wa jiofizikia kwa kutumia ndege (high resolution
airborne geophysical survey) kwa asilimia 16 pekee hivyo bado umuhimu na
uhitaji mkubwa kufanyika tafiti zaidi Ili kuongeza wigo wa maeneo zaidi
yatakayo pelekea kufunguliwa kwa miradi mipya ya uchimbaji madini.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kiruswa amesema Serikali ya
Tanzania kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linawalea wachimbaji
wadogo wa madini kwa kuwapa mafunzo na kuwasaidia kufanya tafiti ili kufanya
shughuli zao kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati wa Marekani Joshua
Volz ameonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika kufanya tafiti zaidi ili
kubaini maeneo mapya yenye viashiria vya madini.
Pia, Volt amesema lengo la ziara yake ni kuona jinsi gani
Serikali ya Marekani inaweza kushirikiana na Tanzania katika uzalishaji wa
madini Mkakati ili kusaidia uzalishaji wa Nishati safi kwa lengo la kupunguza
uharibifu wa mazingira.
Volt amesema Dunia ya sasa inauhitaji mkubwa wa Madini
Mkakati ambapo Serikali ya Marekani ni mdau mkubwa katika uzalishaji na utafiti
wa madini hayo kwa lengo la kupunguza uzalishaji wa Nishati inayoweza
kusababisha hewa ya Ukaa.
0 Maoni