Dkt. Nchimbi achota hekima kwa Dk. Salmin na Dk. Shein

 

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema ushauri na maelekezo ya Viongozi Wastaafu wa Chama, Serikali na Wazee wa CCM kuhusu umuhimu wa kuendelea kukiimarisha Chama, na kuendelea kuwatumikia watu vizuri, yatafanyiwa kazi kwa uzito unaostahili.

Balozi Dk. Nchimbi amesema hayo jana, wakati wa mazungumzo kwa nyakati tofauti na Marais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Wenyeviti wa Baraza la Mapinduzi (wastaafu), Dk. Salmin Amour Juma na Dk. Ali Mohamed Shein, katika makazi yao, na Wazee wa CCM kwenye mikutano yao ya mabaraza, Pemba na Zanzibar. Dk. Salmin na Dk. Shein pia ni Makamu Wenyekiti wastaafu wa CCM.

“Asanteni. Waambie pia nawasalimia. Simamieni Chama…Chama kijengwe, kisimamiwe kupata ushindi mzuri,” amesema Dk. Salmin, baada ya Balozi Dk. Nchini kumpa salaam za Mwenyekiti wa CCM na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussen Ali Mwinyi, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.

Kwa upande wa Dk. Shein, amesisitiza umuhimu wa CCM kuendelea kusimamia misingi ya kuanzishwa kwake.

“CCM ni chama makini sana. Kina misingi na taratibu zake. Na jambo zuri ni kwamba Katibu Mkuu ndiye msimamizi. Nakujua, tumekuwa wote Kamati Kuu na Halmashauri Kuu Taifa ya CCM kwa muda mrefu. Sina shaka nawe kuyasimamia haya. Tukipindisha taratibu tutaanza kwenda kombo. Jengine ni suala la usiri wa vikao, lazima vikao viwe na siri,” amesema Dk. Shein.


Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akimsikiliza kwa makini aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma, wakati wakizungumza, alipomtembelea kwenye makazi yake mjini Zanzibar hapo jana.

Chapisha Maoni

0 Maoni