Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene aridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) huku akiitaka iongeze kasi zaidi katika kusanifu na kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma kwa umma kwa haraka na ufanisi.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo alipokuwa
akizungumza na Watumishi wa eGA-Kituo cha Iringa ambapo amewataka Watumishi hao
kuhakikisha Serikali inaendeshwa kidigitali kwenye kila nyanja kupitia mifumo
wanayoisanifu.
Amesema eGA ni taasisi muhimu katika dunia ya sasa ambapo
Serikali inahitaji mapinduzi ya TEHAMA ili itoe huduma zake kwa wananchi
kiurahisi na kwa haraka.
“Dunia inakwenda kasi na teknolojia ni kila kitu kwa sasa,
hivyo ni muhimu kwa eGA kufanya utafiti, kubuni na kutengeneza mifumo ya TEHAMA Serikalini kwa
ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa umma,” amesema Mhe. Simbachawene.
Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa eGA imeweka juhudi kubwa
katika kusimamia TEHAMA Serikalini na imetengeneza na inaendelea kutengeneza
mifumo ya TEHAMA ambayo imewarahisishia wananchi kupata huduma kwa haraka,
mahali popote na kwa gharama nafuu na kuchagiza utawala bora.
Aidha, Mhe. Simbachawene ameridhishwa na utendaji kazi wa
Mamlaka ya Serikali Mtandao katika ofisi zake zilizopo Iringa na amewataka
watumishi wa Mamlaka kwa jumla kuendelea kubuni Mifumo ya TEHAMA inayotatua
changamoto zilizopo nchini pamoja na kuwa wazalendo kwa maslahi ya Taifa.
Vile vile, amewasisitiza watumishi wa eGA kuhakikisha mifumo
inayotengenezwa na iliyopo inakuwa na uwezo wa kuwasiliana ili kuleta ufanisi
katika kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba amemshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Simbachawene kwa kutenga muda wake kutembelea kituo hicho cha Iringa na kuahidi kutekeleza maagizo yote aliyotoa.
Na. Lusungu Helela- Iringa
0 Maoni