WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU
Mkoa wa Mara, akamilishe uchunguzi kwenye wizi wa kimtandao unaotumika katika
Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
“Kamanda wa TAKUKURU Mkoa fuatilia hili suala kwa haraka, najua
mna tabia ya kufanya uchunguzi wenu kwa muda mrefu. Nataka hili likamilike kwa
haraka kwa sababu nilishatuma timu yangu na kazi kubwa imeshafanyika.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo jioni (Jumatatu, Februari
26, 2024) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda pamoja
na wale wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda uliofanyika kwenye ukumbi wa Herieth,
wilayani Bunda mkoani Mara.
Akizungumza na watumishi hao, Waziri Mkuu amesema Serikali
ina utaratibu wa kukamilisha matumizi ya fedha zilizopangwa ifikapo Juni 30,
kila mwaka. “Ikifika wakati huo, HAZINA wana uwezo wa kuichukua na ikabaki
labda iwe imeandikwa barua ya kuombewa kibali maalum cha kuhamisha fedha kwenda
mwaka unaofuata.”
“Hapa Bunda mnatumia mwanya huo, kuziombea kibali. Kisha
zinahamishiwa kwenye akaunti jumuifu ya amana, halafu zinatolewa na kutumiwa
kinyume na utaratibu.”
Amesema mchezo huo unafanywa na watu wachache kwenye
Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na watumishi wasio waaminifu wa kitengo
cha akaunti jumuifu ya amana kilichopo
OR-TAMISEMI na hata Katibu Mkuu hawezi kujua mchezo huo wala Madiwani pia
hawawezi kujua.
“Mara nyingi wanaocheza mchezo huo hapa Bunda, ni Mkurugenzi
wa Halmashauri, Mweka Hazina na Mkurugenzi wa Mipango wa Halmashauri. Kwa
mfano, mwaka wa fedha 2021/2022 waliomba kibali cha kuhamisha sh. milioni 871.4
ili ziweze kutumika baada ya muda. Lakini walihamisha sh. milioni 962 na
kuzihifadhi huko.”
“Mbali na hizo, kupitia mawasiliano baina ya hawa watatu na
wenzao wa TAMISEMI, zikaingizwa tena sh. milioni 215.3. Je ninyi Waheshimiwa
Madiwani mliziomba hizo fedha? Je mlijulishwa kwamba kuna fedha za ziada
zimeombwa?” alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa hapana na madiwani waliokuwepo.
Waziri Mkuu amesema kibaya zaidi, fedha hizo zinapotoka,
zinaelekezwa kwenye kazi ambazo tayari zilishatengewa vifungu na ambazo tayari
ziliombewa kibali. “Walitoa fedha na kuandika zimetumika kwenye jengo la
utawala, kutengeneza fedha za hesabu za mwaka, jengo la wagonjwa wa dharura,
posho ya kujikimu ya walimu wapya wa shule za msingi. Hizi zote zilikuwa na
fedha zake, je zimeenda wapi?”
“Kamanda wa TAKUKURU, nataka ufuatilie ni nani aliomba hizo
sh. milioni 215.3? Ni kwa nini fedha hizi zitumike kwenye kazi ambazo tayari
zina mafungu yake? Je ni kweli hawa walimu walilipwa hizo posho? Kwa nini
madiwani hawakujulishwa kuhusu mchakato wa fedha hizi?”
Waziri Mkuu anaendelea za ziara yake mkoani Mara kwa
kuhutubia wakazi wa Mji wa Bunda.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni