Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Mhandisi Anthony Sanga amewataka watumishi wa sekta ya ardhi kutokuwa chanzo
cha migogoro ya ardhi na badala yake wawe wasuluhishi wa migogoro hiyo.
Aidha, amewataka watumishi wa sekta hiyo kufanya kazi kwa
uadilifu na weledi katika kutimiza majukumu yao bila kusahau kuzingatia sheria,
kanuni, miongozo na taratibu.
Mhandisi Sanga ametoa kauli hiyo tarehe 9 Februari 2024
wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi pamoja
na kuzungumza na watumishi wa sekta ya ardhi mkoani Tabora.
Vile vile, kiongozi huyo alikagua miradi inayotekelezwa na
Chuo Cha ardhi Tabora ( ARITA) pamoja na kujadili changamoto zinazokikabili
chuo hicho.
Amewaasa watumishi hao wa sekta ya ardhi kuhakikisha kuwa,
wanatoa majibu yenye uhakika kwa wateja na sio kuwazungusha pale wanapohitaji
huduma za ardhi.
"Mhakikishe mnatoa majawabu ya uhakika kwa wananchi
badala ya kuwapiga danadana na kuwazungusha bila sababu. Mwananchi ajisikie
kuwa kuhudumiwa vizuri katika sekta ya ardhi siyo anasa bali ni haki yake,"
alisema Mhandisi Sanga.
Aidha, amewataka watumishi hao kujenga tabia ya kuonyana
wenyewe kwa wenyewe pindi mmoja wao anapokwenda kinyume na kanuni za utumishi
wa umma.
Akigeukia suala la kodi ya ardhi, mhandisi Sanga amesisitiza
suala la ukusanyaji mapato kupitia kodi
ya pango la ardhi na kuwataka makamishna wa ardhi wasaidizi kote nchini
kulisimamia jambo hilo kikamilifu kwa kuweka mikakati madhubuti.
Kwa upande wa Chuo cha Ardhi Tabora, ameutaka uongozi wa
Chuo hicho kukaa na kutafakari ni namna gani watakuja na mipango ya maboresho
ya kimitaala na miundombinu ya chuo ili kiweze kujiendesha katika hali ya
ushindani na vyuo vingine.
Ameweka wazi kuwa, ataunda timu ndogo itakayokuwa na jukumu la kukaa na kutafakari na hatimaye kuja na mapendekezo ya kuboresha chuo hicho.
Na. Munir Shemweta- WANMM
0 Maoni