Lowassa afariki dunia, maombolezo siku tano

Waziri Mkuu Mstaafu Edward Ngoyai Lowassa amefariki dunia leo Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Muhimbili Jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

Akitangaza taarifa ya kifo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema kwa masikitiko makubwa rais anatangaza kifo cha Lowassa kilichotokea leo majira ya saa nane mchana.

Dkt. Mpango amesema Lowassa ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 70, alikuwa akipatiwa matibabu ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu pamoja na shinikizo la damu.

Amesema Lowassa aliuugua kwa muda tangu Januari 24, 2022 na kutibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na baadae alipelekwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu kabla ya kurejea tena taasisi ya JKCI.

Kufuatia kifo hicho cha mwanasiasa huyo mkongwe na maarufu mno katika siasa za Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan, ametangaza siku tano za maombolezo na bendera zitapeperushwa nusu mlingoti.


Chapisha Maoni

0 Maoni