Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia-WB, wanaendelea na
majadiliano ya namna ya utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya kidijitali, ambapo
wataalam kutoka katika Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutoka Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi, Zanzibar pamoja na taasisi mbalimbali za Umma, wamekutana mjini
Zanzibar kwa ajili ya majadiliano hayo.
Mradi huo unatarajia kutekelezwa kwa gharama ya dola za
kimarekani milioni 150 sawa na shilingi Bilioni 348 za kitanzania na
unatazamiwa kuboresha na kuimarisha huduma za mawasiliano nchini.
Ni katika mkutano wa tatu wa kikao cha utekelezaji wa
Tanzania ya Kidijitali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ulioanza februari 19 hadi
23 mwaka huu mjini Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo
utajadili malengo ya kuongeza upatikanaji wa huduma za mtandao wa intaneti
zenye gharama nafuu na ubora wa juu kwa serikali, wafanyabiashara na wananchi
sambamba na kuboresha uwezo wa serikali wa kutoa huduma za umma kidijitali.
Akizungumza wakati akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara
ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bi.
Khadija Khamis Rajab, amesema matarajio ya serikali ni kwamba miradi ya
kimkakati katika sekta ya mawasiliano itatekelezwa.
“Tunatarajia mradi huu utaenda kutekeleza mambo makubwa ili
tuweze kutekeleza miradi mingine ya kimkakati katika sekta yetu hii ya
mawasiliano, tuna maeneo mengi ya msingi ambayo yatakuwa yamegawanywa katika
mradi huu wa Tanzania ya kidijitali, na katika maeneo hayo kutakuwa na maeneo
makuu matatu ambayo ni pamoja na kupitia na kuhuisha sheria miongozo na
taratibu za kisheria za TEHAMA ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia”
amesema Ndugu. Rajab.
Meneja wa mradi huo wa Tanzania ya Kidijitali Bw. Bakari
Mwamgugu amesema pia kutakuwa na maboresho ya miundombinu ya TEHAMA, ikiwepo
kuunganisha taasisi za serikali katika mkongo wa mawasiliano taifa, kuboresha
vituo vya kuhifadhia kanzidata, na kupeleka mawasiliano katika maeneo ambayo
hakuna mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuboresha mawasiliano kutoka 2G kwenda
4G.
“Lengo la tatu ni kuboresha na kutekeleza mifumo mbalimbali
itakayosaidia kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa wakati, ukiwepo mfumo wa
jamii namba, ambao kila mtanzania atatakiwa kuwa na namba moja tu ya kupata
huduma,” amesema Bw. Bakari.
Mradi huo una malengo ya kuongeza upatikanaji wa huduma za
mtandao wa intaneti zenye gharama nafuu na ubora wa juu kwa serikali,
wafanyabiashara na wananchi, sambamba na kuboresha uwezo wa serikali wa kutoa
huduma za umma kidijitali.
Mradi wa ‘Tanzania ya Kidijitali' unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unatekelezwa kwa usimamizi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali zinazohusika na TEHAMA kwa upande wa Tanzania Bara na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Na. Grace Semfuko- MAELEZO
0 Maoni