Bodi ya Nishati Vijijini (REB) inayosimamia Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), imesema inategemea mafanikio makubwa katika kuiwezesha
Wakala hiyo kutimiza azma yake ya kuwafikishia wananchi walioko vijijini
nishati bora za umeme, mafuta na gesi.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Bodi
hiyo, Balozi, Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu baada ya kikao cha kwanza cha
Bodi hiyo mpya kilicholenga kutambuana na kupanga majukumu.
“Kikao chetu kimeenda vizuri, tumechagua Kamati na
kupangiana majukumu. Tunaamini na tunaahidi kuwa tutatekeleza majukumu yetu
sawasawa na Sheria iliyoanzisha Wakala wa Nishati Vijijini inavyoelekeza,”
amesema.
Aidha, Balozi Kingu amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu
Hassan kwa kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi na amemshukuru Naibu Waziri Mkuu
ambaye pia ndiye Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko kwa
kukamilisha mchakato wa uteuzi wa Wajumbe wa Bodi, jambo ambalo limeiwezesha
kuwa Bodi kamili.
Akieleza zaidi kuhusu majukumu waliyojipangia, Balozi Kingu
amesema mapema Mwezi Machi, Bodi itakutana katika kikao cha dharura kupitia na
kujadili masuala mbalimbali ya Wakala ambayo yalikuwa yakisuburi baraka za Bodi
ili kuyatolea maamuzi yatakayowezesha utekelezaji wake kwa manufaa ya wananchi
na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Katibu wa Bodi hiyo ambaye pia ni
Mkurugenzi wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amepongeza Mamlaka za Uteuzi, kuteua
watu makini, hodari na wachapakazi ambao amesema ni muhimu kuwa nao katika
kuisimamia Wakala hiyo yenye majukumu makubwa yanayogusa maisha ya wananchi
moja kwa moja.
“REA ina jukumu kubwa ambalo linagusa maisha ya watu lakini
pia linahusisha kiasi kikubwa sana cha fedha za Serikali. Kwahiyo, kuwa na Bodi
nzuri iliyosheheni watu makini, kwetu sisi ni jambo la faraja,” amefafanua.
Mkurugenzi Mkuu, kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi
wote wa REA, ametoa ahadi ya ushirikiano kwa Bodi hiyo mpya ili kuhakikisha
malengo ya Serikali kupitia majukumu yaliyokasimiwa kwa Wakala yanatekelezwa.
“Tunatamani kuona Watanzania wenzetu wanaoishi vijijini
wanapata nishati bora kama ilivyo kwa wenzao wanaoishi mjini,” amesisitiza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wajumbe wa Bodi
wamezishukuru Mamlaka za Uteuzi kwa kuwaamini na kuwapa jukumu hilo kubwa la
kuisimamia REA ili kuendelea kuleta matokeo chanya.
Aidha, wamepongeza Bodi zilizotangulia kabla yao,
Menejementi pamoja na Wafanyakazi wote kwa kazi nzuri waliyofanya tangu
kuanzishwa kwa Wakala na kuahidi kuendeleza yote mazuri yaliyofanyika ili
kuongeza tija.
Kikao hicho pia kilishirikisha Menejimenti ya Wakala ambapo Wakuu wa Idara na Vitengo waliwasilisha kwa Bodi taarifa za utekelezaji wa majukumu katika maeneo wanayosimamia kwa lengo la kuijengea Bodi uelewa na ufahamu kuhusu Taasisi hiyo waliyopewa jukumu la kuisimamia.
Januari 26 mwaka huu, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri
wa Nishati, Dkt. Doto Biteko aliwateua Florian Otman Haule, Lucas Charles
Malunde, Mwantum Issa Sultan, Stephen Menard Mwakifamba, James Issack Mabula,
Ahmed Martin Chinemba, Sophia Shaban Mgonja na Balozi Radhiya Naima Msuya kuwa
Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, wakiungana na Balozi Meja Jenerali Mstaafu
Jacob Gideon Kingu aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,
Septemba 2023 kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo.
Na Veronica Simba-
REA
0 Maoni