WAZIRI MKUU na Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Kassim Majaliwa amesema Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kinara katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha
Mapinduzi.
“Ni ukweli usiopingika kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama chetu
amekuwa kielelezo cha mafanikio makubwa yanayofikiwa na nchi yetu kwa sasa.”
Amesema tangu Dkt. Samia ashike madaraka ya Urais,
ameendelea kutekeleza miradi yote ya kimkakati kama Ilani ya CCM ya mwaka
2020-2025 ilivyoelekeza.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo jana katika Mkutano Mkuu
wa CCM Jimbo la Kavuu, uliofanyika kwenye shule ya sekondari ya Mizengo Pinda
iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, katika Wilaya ya Mlele, mkoani
Katavi.
“Dkt. Samia Suluhu
Hassan ameendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ikiwemo
upatikanaji wa huduma za afya, kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa, Kanda na rufaa.”
Amesema pamoja na mafanikio mengine, Rais Samia ameimarisha
diplomasia ya kiuchumi na nchi mbalimbali sambamba na kukuza utalii, lugha ya
Kiswahili na masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania waendelee
kukiamini Chama cha Mapinduzi kwani wakati wote kimeendelea kuwa nguzo ya
kuwaunganisha Watanzania katika kujenga Taifa linalojitegemea kiuchumi, kisiasa
na kiutamaduni, na Taifa lenye umoja, amani, utulivu na mshikamano.
“Taifa hili, chini ya Serikali za CCM tuna uwezo mkubwa wa
kujitegemea na kujiletea maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii. Haya
yamedhihirika kupitia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ujenzi wa Taifa
letu na kuboresha maisha ya Watanzania katika nyanja mbalimbali.”
Amesema Chama cha Mapinduzi kimekuwa nguzo ya amani, umoja
na mshikamano miongoni mwa Watanzania na hivyo kuwa chachu ya maendeleo nchini.
“Umuhimu wa chama chetu, umeendelea kuonekana kwa jinsi ambavyo kimekuwa
kikiwatumikia Watanzania huku nchi yetu ikidumisha umoja na amani miongoni mwa
wananchi.”
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geoffrey Pinda alisema Jimbo la Kavuu na
Halmashauri ya Mpimbwe kwa ujumla wamepiga hatua kubwa katika utekekezaji wa
Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye sekta za afya, elimu, miundombinu na
maendeleo ya jamii.
Amesema, zaidi ya shilingi bilioni 1.2 zimetolewa kugharamia
elimu bila malipo na shilingi milioni 238 zimetumika kukarabati shule kongwe.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, alisema
shilingi bilioni 800 zimepokelewa kwa kwa ajili ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM
na kuahidi kuwa wataendelea kusimamia Ilani hiyo pamoja na fedha zinazoletwa na
Serikali kutekeleza miradi mbalimbali.
Awali, akiwa njiani kuelekea Mpimbwe, Mheshimiwa Majaliwa
alisimama na kuzungumza na wananchi wa eneo la Sitalike ambapo pamoja na mambo
mengine, amewasihi wawe wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kutatua mgogoro
wa ardhi katika eneo hilo.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni