WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuongoza Mazishi ya Waziri Mkuu Mstaafu Hayati
Edward Lowassa yanayotarajiwa kufanyika Wilayani Monduli Mkoani Arusha Jumamosi
Februari17, 2024.
Awali Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitangaza
siku tano za maombolezo ya kitaifa ambapo bendera zitapeperushwa nusu mlingoti
kuanzia tarehe 10 Februari, 2024.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana wakati akitoa taarifa ya ratiba ya mazishi ya kiongozi huyo, Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu Oysterbay, Dar es Salaam.
Amesema katika kipindi cha siku tano za maombolezo, Taifa
litaendelea na shughuli za umma na kijamii sambamba na kushirikiana na
wanafamilia katika ratiba ya msiba kama ilivyoandaliwa na kamati ya mazishi ya
Kitaifa na wanafamilia.
Amesema kabla ya mazishi hayo mwili wa Hayati Lowassa
unatarajiwa kuagwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na Sheikh
Amri Abeid jijini Arusha.
Amesema Jumanne Februari 13, 2024 mwili wa Hayati Lowasa
unatarajiwa kuangwa na viongozi na wananchi katika viwanja vya Karimjee jijini
Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Jumatano Februari 14 mwili wa Hayari
Lowasa utapelekwa katika Kanisa la KKKT Azania Front kwa ajili ya ibada
takatifu na kuaga.
Amesema Alhamisi Februari 15 mwili wa Hayati Lowassa
utasafirishwa hadi jijini Arusha ambapo viongozi na wananchi watapa fursa ya
kuaga katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid.
Waziri Mkuu huyo mstaafu alifariki juzi (Jumamosi, Februari 10, 2024) wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam na tangazo la kifo chake lilitolewa na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni