Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kusainiwa kwa sheria mpya itaondoa changamoto
ambazo zilikuwa vikwazo katika kufikia malengo ya kimaendeleo.
Amesema sheria hizo mpya ni Sheria mpya ya Mahkama ya Kadhi
Zanzibar, Sheria mpya ya Ukaguzi wa Umma, Sheria mpya ya Uwekezaji Zanzibar,
ambayo ni sheria bora kwa mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji nchini, Sheria
ya kuweka masharti ya utoaji leseni
udhibiti na usimamizi wa huduma ndogo za fedha kwa ajili ya kudumisha utulivu,
usalama na ubora wa huduma hizo.
Rais Dk. Mwinyi amesema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini
wa sheria mpya nne viwanja vya Ikulu Zanzibar tarehe: 01 Februari 2024.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi amesema Sheria zilizosainiwa zimepita
katika hatua mbalimbali ikiwemo kufanyika kwa utafiti wa kina na ukusanyaji wa
maoni ya wadau Unguja na Pemba kabla ya kuwasiilishwa Baraza la Wawakilishi na kujadiliwa kwa mfumo
wa demokrasia shirikishi.
Halikadhalika Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuwa ni jambo la
kihistoria kusainiwa kwa sheria mpya nne hadharani kwa wakati mmoja.
Kwa upande mwingine Rais Dk. Mwinyi amesema Sheria zote nne
zilizosainiwa zinagusa moja kwa moja maslahi ya wananchi na haki zao ikiwemo
kuimarisha miongozo ya mifumo jumuishi ya
kusimamia shughuli zote za uwekezaji, kupanua wigo wa kazi za
ukaguzi ili kufikia ngazi za kitaifa na
kimataifa, kubaini na kuzuia matumizi mabaya ya fedha za umma, kukabiliana na
vitendo vya rushwa, kuzuia matumizi
mabaya ya mifumo inayoathiri utekelezaji wa kazi za ukaguzi.
Rais Dk. Mwinyi amezitaka taasisi za sheria kufanya mapitio sheria zinazokwaza kasi ya maendeleo katika maeneo ya mafuta na gesi asilia.
0 Maoni