Mloganzila yaondoa bandama kwa kutumia tundu dogo

 

Hospitali ya Taifa Muhimbli Mloganzila kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa kutoka Korea Kusini imeandika historia nyingine tangu kuanzishwa kwa kufanya huduma ya kuondoa bandama kwa kutumia matundu madogo kwa mgonjwa aliyekuwa na bandama kubwa ambalo lilikuwa liina muathiri kwa muda mrefu.

Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa Bobezi wa Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini MNH-Mloganzila, Dkt. Richard Mliwa alipokuwa akielezea namna walivyoweza kufanikisha huduma hiyo kwa mafanikio.

Dkt. Mliwa ameongeza kuwa huduma ya matundu ina manufaa makubwa ambayo ni pamoja na mgonjwa kutopata maumivu makali, mgonjwa kutokuwa na kidonda kikubwa kwakuwa haihusishi kupasuliwa, mgonjwa kurejea katika majukumu yake ya kila siku mapema zaidi ukilinganisha na huduma ya kupasua.

“Huduma hii tumeifanya kwa mafanikio makubwa na kwa kutumia muda mdogo na itakuwa endelevu kwakuwa tuna miundombinu, vifaa tiba na wataalamu bobezi katika kutoa huduma hizi katika hospitali yetu,” ameongeza Dkt. Mliwa.

Aidha, Dkt. Mliwa amebainisha kuwa miongoni mwa dalili zinazopelekea mgonjwa kuhisi anahitaji kuondolewa bandama ni pamoja na bandama kuwa kubwa ambapo akishika tumbo anahisi ukubwa huo, kuwa na dalili za upungufu wa damu ikiwemo kizunguzungu na kichwa kuuma.

Dkt. Mliwa ameongeza kuwa kama bandama halitaondolewa kwa wakati mgonjwa anaweza kupata changamoto mbalimbali ikiwemo bandama kuwa kubwa, mwili kushindwa kugandisha damu kutokana na upungufu wa chembe sahani na mgonjwa kuhisi maumivu makali.

Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila kwa siku za karibuni imejipanua katika kutoa huduma za upasuaji wa kutumia matundu madogo na hivyo kuwa kimbilio kwa Watanzania wengi ambao walikuwa wanaenda nje ya nchi kutafuta huduma za aina hii.

Chapisha Maoni

0 Maoni