Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Rajab Telack amewataka
wakazi wa wilaya ya Kilwa na Mkoa wa Lindi kwa ujumla kuwa tayari kuwapokea
watalii wanaotembelea Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na
Songo Mnara na kutumia fursa hiyo kufanya biashara za bidhaa za utalii ili
kuwaingizia kipato.
Mhe. Zainab ameyasema hayo jana Februari 28, 2024 akiongea na
waandishi wa habari ndani ya Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa
kisiwani na Songo Mnara wakati wa mapokezi ya Meli ya Saba kuingia Hifadhini
humo katika kipindi cha mwezi Februari ikiwa na idadi ya watalii 120 kutoka
Mataifa mbalimbali Duniani.
Amesema mfululizo wa safari za Meli za watalii ndani ya
Hifadhi hiyo ni kiashiria kwamba filamu ya Tanzania The Royal Tour iliyochezwa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
imeleta matokeo chanya kwa Mkoa wa Lindi na Tanzania kwa ujumla.
Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa Hifadhi ya Urithi wa
Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara iliyo chini ya usimamizi wa
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA inatarajia kupokea Meli
nyingine zaidi za watalii Mwezi Machi na April hivyo wakazi wa Mkoa huo watumie
vyema ujio wa Meli hizo.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwaalika watu wote wenye bidhaa
zinazopendwa na watalii na kuziuza wakati wa safari za wageni ndani ya Hifadhi
hiyo huku akisisitiza kuwa TAWA imejenga
jengo la kisasa na maalumu kwa ajili ya wafanyabiasha wa bidhaa za kitalii,
hivyo walitumie jengo hilo ipasavyo.
Akibainisha sababu za watalii wengi kutembelea Hifadhi ya
Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mkuu wa Hifadhi hiyo Mercy
Mbogelah amesema majengo ya kale yaliyojengwa zaidi ya miaka 1000 iliyopita
kama vile msikiti mkubwa na mkongwe kuliko yote katika ukanda wa Pwani ya
Afrika Mashariki na ngome ya Mreno ni vivutio vikubwa vya watalii
vinavyowafanya watalii wengi kumiminika katika Hifadhi hiyo
Amesema kutokana na historia hiyo kubwa ndani ya Hifadhi ya
Kilwa kisiwani Mwaka 1981 Shirika la
Kimataifa la UNESCO liliipa hadhi Hifadhi hiyo na kuwa Hifadhi ya Urithi wa
utamaduni wa Dunia na baadae Mwaka 2023
kuwepa hadhi nyingine kuwa "Man and Biosphere Reserve". Vigezo
vyote hivi vimetajwa kuwa mojawapo ya sababu za watalii wengi kutoka nje
kupenda kuitembelea.
Maboresho ya
miundombinu wezeshi ya utalii yaliyofanywa na Serikali kupitia TAWA nayo
imetajwa kuwa miongoni mwa sababu za watalii wengi wa ndani na nje kupenda
kutembelea na Kutalii ndani ya Hifadhi hiyo.
Naye Afisa Utalii wa Hifadhi hiyo, Shindawangoni Rajabu amesema
Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara imekuwa
ikipokea Meli kubwa za watalii na Mwaka huu wa 2024 imepokea Meli nyingi zikiwa
na idadi kubwa ya watalii katika kipindi kifupi ikilinganishwa na miaka mingine
yote na inatarajia kuendelea kupokea Meli nyingine zaidi za watalii kutoka
Mataifa mbalimbali Duniani.
Amesema ongezeko la idadi ya Meli zenye idadi kubwa ya watalii ni kiashiria tosha kuwa Hifadhi hiyo inaendelea kivutio kizuri zaidi Duniani.
Na. Beatus Maganja
0 Maoni