Jeshi la Polisi linamshikilia mwanamke aliyejianika uchi Zanzibar

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linawashikilia watuhumiwa watatu kwa kufanya kitendo chenye maudhi kwa jamii.

Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Richard Thadei Mchomvu wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Madema.

Amefafanua kuwa, hivi karibuni kulisambaa video clip ikionesha mwanamke anavua nguo na kuonesha sehemu zake za siri akiwa amepakiwa kwenye pikipiki yenye namba za usajili Z.455 LN aina ya TVS.

Kamanda Mchomvu alieleza kwamba, baada ya kufanya uchunguzi wa kina walibaini kwamba tukio hilo lilitokea tarehe 16 Februari 2024 majira ya saa 11:00 alfajiri.

"Tulifanya uchunguzi ambapo mnamo tarehe 22 Februari 2024 tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote watatu," alisema Kamanda Mchomvu.

Amewataja watuhumiwa waliokamatwa ni Mohd Shaib Mohd (35) mkaazi wa Magomeni ambaye ni dereva wa pikipiki, Sabrina Samwel Thomas (21)  na Asia Salum Juma (23) mkaazi wa Shakani ambaye alionekana kuvua nguo hadharani katika video hiyo jambo ambalo ni kosa kisheria.

Sambamba na hayo, Kamanda Mchomvu ameeleza kuwa, dereva wa pikipiki hiyo aliendesha chombo hicho bila kuzingatia sheria za usalama barabarani kwa kuwabeba abiria wawili bila kuvaa kofia ngumu na kuendesha pasipo kuzingatia usalama wake na watumiaji wengine wa barabara.

Aidha, Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa madereva wasiotii sheria za usalama barabarani.

"Huyu dereva tutamchukulia hatua kali za kisheria ikiwa pamoja na kuiomba Mamlaka zinazohusika zimfungie leseni yake ili iwe mfano kwa madereva wengine wasiofuata sheria na kutii maadili ya nchi yetu," aliongeza Kamanda Mchomvu.

Upelelezi wa tukio hilo unaendelea na utakapokamilika, watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Chapisha Maoni

0 Maoni